Rayvanny aachia collabo ya kwanza na msanii wa kimataifa baada ya kuondoka WCB

Rayvanny alitangaza kuwa baada ya kuondoka WCB anaachia collabo yake na msanii @luanavjollca

Muhtasari

• Rayvanny aliondoka rasmi wasafi wiki jana katika tukio lilizozua joto kali mitandaoni ambalo mpaka sasa vumbi yake haijapoa.

Msanii mkurugenzi wa lebo ya Next Level Music, Rayvanny
Msanii mkurugenzi wa lebo ya Next Level Music, Rayvanny
Image: Instagram//Rayvanny

Chawa wa lebo ya WCB Wasafi, Baba Levo amefichua kwamba wiki moja baada ya Rayvanny kuondoka rasmi Wasafi, sasa anatarajiwa kuachia collabo yake ya kwanza kama msanii huru nje ya wasafi.

Baba Levo alisema Rayvanny anatarajiwa kuachia collabo hiyo kwa jina PelePele na msanii wa kimataifa kwa jina @luanavjollca.

“Vanny boy @rayvanny pelepele. Asishindanishwe kabisa na takataka. Huyu ni wa kimataifa,” Baba Levo alisema.

Msanii Rayvanny alionekana kukiri ujio wa hii collabo ambapo alimsifia Baba Levo na kumuita mshua wa moja kwa moja asiyebahatisha katika maneno yake. Rayvanny alifichua kwamba mzalishaji S2Kizzy ndiye atakuwa nyuma ya midundo ya kiuhakika kabisa kweney mradi huo wa PelePele.

Wiki jana, Rayvanny alitangaza kuondoka Wasafi baada ya kuhudumu miaka sita katika lebo hiyo kubwa kabisa ukanda wa Afrika Mashariki.

Tukio la kuondoka kwake liligubikwa na maneno mengi huku baadhi wakitema kashfa na wengine wakiupongeza uamuzi wake wa kuondoka bila tafashi.

Watu wengi akiwemo mzalishaji wa zamani wa ngoma P Funk Majani ambaye alikuwa mpenzi wa Kajala Masanja kwa wakati mmoja amekuwa wa hivi punde kusema kwamba wasanii wanaondoka Wasafi kwa sababu ya unyanyaswaji kwa maslahi yao, akitolea mfano Harmonize ambaye aliondoka miaka mitatu iliyopita na kunawiri baada ya kujisimamia binafsi, na pia Rayvanny ambaye amegura juzi.

Diamond amejitokeza na kutetea lebo yake dhidi ya kashfa za kuwafyonza wasanii na kusema kwamba wasanii wenyewe wakiingia mule huwa kuna mikataba na baada ya wao kuona pesa zimeanza kuingia, wengi hutaka kuondoka.

Pia, Simba alisema kwamab inakuwa furaha yake kuona wasanii aliowakuza wakiota mabawa na kutaka kuondoka ili pia kujijenga na kuwashika mkono wengine katika Sanaa, jambo ambalo alisema linampa motisha sana akiona wasanii aliowakuza kama Harmonize wakifanya vizuri mno katika safari ya muziki nje ya Wasafi.