Staa wa R&B na Soul, Anthony Hamilton afunguka kuhusu maisha Marekani na kazi ya muziki

Hamilton anaishi katika eneo la Charlotte na amebarikiwa kuwa na familia ya watoto sita.

Muhtasari

• Hamilton alianza muziki akiwa na umri wa miaka 17 ambapo alikuwa anaimba kwenye kwaya ya shule ya upili.

• Mwaka 2000 alitambulishwa rasmi kwenye muziki wa biashara na safari yake ikang'oa nanga ambapo mwaka 2009 alishinda tuzo ya Grammy.

• Hamilton alioa mmoja wa waimbaji katika kikundi chake mwaka 2005 lakini walitangaza kuachana mwaka 2015, baada ya miaka 10 kwenye ndoa.

Gwiji wa miziki ya RnB na Soul, Anthony Hamilton
Gwiji wa miziki ya RnB na Soul, Anthony Hamilton
Image: Instagram//anthony hamilton

Mshindi wa tuzo ya Grammy, muimbaji na mtunzi wa ngoma za Soul na RnB, Anthony Hamilton raia wa Marekani anatarajiwa kutumbuiza kwenye tafrija kubwa ya Stanbic Yetu Festival.

tarehe 30 mwezi huu wa Julai katika ukumbi wa Carnivore jijini Nairobi, tamasha ambalo linaandaliwa kwa ufadhili wa benki ya Stanbic kwa kushirikiana na shirika la habari la Radio Africa Group.

Lakini je, unafahamu Anthony Hamilton ni nani? Vipi kuhusu maisha yake Amerika kama Mmarekani mweusi? Na kazi yake ya muziki je? Bila shaka, hapa maswali yote tutapata kukujuza baada ya Hamilton kutuchukua katika safari ya kupata majibu kamili kumhusu kwa undani zaidi.

Safari ya muziki

Anthony Hamilton alizaliwa mnamo mwaka wa 1971 katika eneo la Charlotte, Carolina Kaskazini huko Marekani. Safari yake ya muziki ilianza katika umri mbichi kabisa wa miaka 17 akiimba katika kanisa ambapo pia alikuwa mmoja wa wanakwaya wa shule ya upili ambayo ilishinda tuzo mwaka 1992.

Baada ya kumaliza shule ya upili, alishirikishwa na wasanii tajika kipindi hicho kama muimbaji wa akiba katika tamasha mbali mbali ambapo mwaka wa 1999 alishirikiana kuandika kibao cha ‘U Know What’s Up’ yake msanii Donell Jones, na ikawa moja wa vibao moto sana kuingia miaka ya 2000.

Msanii huyo anayeshabikiwa sana kwa mtindo wa RnB nchini Marekani alipata umaarufu wake katika fani ya muziki baada ya albamu yake ya pili kufanya vizuri katika mauzo ya kiwango cha platinamu mnamo mwaka wa 2003, albamu iliyokwenda kwa jina Comin’ From Where I’m From, mafanikio ambayo yalimpa umaarufu na baadae kuteuliwa kuwania tuzo za Grammy kwa  17.

Kabla ya umaarufu huo, Hamilton anakumbuka mara ya kwanza kutambulishwa kwa umati wa mashabiki mwaka wa 2002 ambapo aliimba kiitikio cha ngoma ya msanii Nappy Roots, kwa jina Po’ Folks, ngoma ambayo ilipata kuteuliwa kwenye tuzo za Grammy katika kitengo cha Best Rap/Sung collaboration.

Baada ya upenyo huo mkubwa kwenye gemu la wakubwa, Hamilton alizidi kuachilia vibao moto katika ubora wake ambapo mwaka wa 2006 alishinda tuzo ya BET kwenye mradi wa Cool Like That, na kushirikishwa katika kibao cha So In Love kutoka kwa msanii Jill Scott mwaka wa 2011, kibao ambacho kiliweka rekodi ya kusalia kileleni mwa chati za Urban AC kwa wiki 19 mtawalia.

Miaka hiyo yote, gwiji huyu alizidi kushirikishwa na kuwashirikisha wasanii kadha wa kadha katika miradi ya miziki ambayo ilifanya vizuri mno kwenye majukwaa mbali mbali na kulipa jina lake heshima ya kutukuka pakubwa.

Mnamo mwaka 2016, Hamilton alizindua albamu yake ya sita kwa jina What I’m Feelin’ ambayo katika mahojiano alisema ni moja kati ya albamu zake ambayo ina hisia nyingi zinazoyatafakari yote ambayo ameyapitia katika maisha yake ya nyuma.

Mwaka wa 2017, msanii huyo kwa mara nyingine tena aliandikisha historia baada ya kushirikishwa kwenye collabo na kundi la Gorillaz kwenye kibao cha Carnival ambacho ni moja ya vibao vilivyofanya vizuri kutoka albamu ya Humanz.

Mwaka wa 2020 wakati janga la Corona lilizua taharuki ulimwengu kote, Hamilton aliingia studioni na kuachilia kibao chake kimoja Back Together ambacho alimshirikisha Rick James, kibao ambacho iligundulika ni moja katika albamu yake ya saba kwa jina Love Is The New Black ambayo alizindua mwezi Septemba mwaka 2021.

Mpaka sasa, maisha ya kimuziki ya msanii huyu yamekuwa ya kufana mno ambapo tangu mwaka wa 2003 baada ya albamu yake ya kwanza amekuwa akiteuliwa kuwania tuzo mbali mbali na mwaka 2006, Hamilton aliteuliwa na kushinda tuzo ya BET J Cool Like Dat na pia kubwa zaidi ni ile tuzo ya Grammy ya mwaka 2009 aliyoshinda katika kitengo cha Best Traditional RnB & Performance kutokana na kibao You’ve Got The Love I Need, collabo aliyoshirikisha msanii Al Green.

Maisha Marekani

Kando na umaarufu wa kimuziki, Hamilton pia ni baba wa familia ambapo ana watoto 6 na wote wanaishi Marekani. Hamilton alioa mmoja wa waimbaji wake wa akiba kwa jina Tarsha McMillan mwaka 2005, hata hivyo baada ya miaka kumi kwenye ndoa, mwaka wa 2015 walitangaza kutalikiana.

Mwanamuziki huyo ni Mkristu na alisema anawafunza wanawe mambo ya dini sana ili kua katika makuzi ya ukweli na uwajibikaji kwa mambo yaliyo mema.

Kulingana naye, mapenzi yake kwa eneo la Charlotte, ambako alizaliwa na kulelewa bado linabaki kuwa moja ya sehemu zenye upendo mkubwa moyoni mwake na kusema kwamba eneo hilo lina mandhari mazuri ya kukuza familia na ndio maana baadae aliamua kurudi huko baada ya kuondoka kwenda mjini New York kwa ajili ya muziki. Alisema eneo hilo lina watu wenye mawazo wazi na sasa lishakuwa kubwa zaidi kama mji.

Msanii huyo alisema licha ya kuwa Mmarekani mwenye ngozi nyeusi bado muziki wake umekuwa ukipata mapokezi mazuri si tu Marekani bali kote ulimwenguni na hili linampa msukumo wa kufanya vizuri hata zaidi katika tasnia hiyo ambayo sasa imejawa na ushindani mkali.

Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa tamasha kubwa la Stanbic Yetu Festival kufanyika kwani mwaka wa 2020 wakati wa janga la Corona, tafrija hiyo ilifanyika kupitia mitandao ya kijamii mwezi Agosti 2020 wakati wa kafyu kutokana na janaga la COVID-19. Tafrija hiyo ya kidijitali ililenga kuunganisha jumuiya ya muziki ya ndani na kimataifa wakati wa janga hili.

 

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO.