Dadake Betty Kyallo arusha bonge la tafrija kusherehekea ujauzito wa mbwa wake

Dadake Betty Kyallo, Gloria Kyallo alizua mjadala mitandaoni baada ya kuandaa tafrija ya kusherehekea 'Puppyshower' ya mbwa wake.

Muhtasari

• “Washerehekee Wanyama wenu kwa sababu wao ndio huwa na mapenzi ya kitiifu kikweli,” Gloria aliandika.

• “Yaani mbwa anafanyiwa party Mimi hata keki sijaipata moja ikona jina langu,” mmoja kwa jina Ivy Leaky aliandika.

Mwanaharakati wa afya ya akili ya wanyama, Gloria Kyallo
Mwanaharakati wa afya ya akili ya wanyama, Gloria Kyallo
Image: Instagram//gloriakyallo

Dadake mwanahabari maarufu nchini Betty Kyallo, Gloria Kyallo amesimamisha mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia leo baada ya kupakia picha na video kwenye Instagram yake akisema kwamba alikuwa anaandaa sherehe za kukaribisha mtoto wa mbwa wake ambaye ni mjamzito, kwa lugha ya kimombo ‘Puppyshower’ kutoka kwa ile ya binadamu ya ‘Babyshower’

Kulingana na picha hizo, bila shaka Kyallo aliarusha tamasha la kifahari ambalo lilihudhuhiriwa na marafiki wake wa karibu kusherehekea ujauzito wa mbwa huyo wake aina ya Chiwawa.

Akitetea hatua yake, Gloria Kyallo aliwataka mashabiki wake waliokuwa wanamsimanga kwa kuandaa tafrija kwa ajili ya uzauzito wa mbwa kwa kuwaambia kwamba si vibaya kuwasherehekea Wanyama kwani huwa wanaonesha binadamu mapenzi ya dhati.

“Washerehekee Wanyama wenu kwa sababu wao ndio huwa na mapenzi ya kitiifu kikweli,” Gloria aliandika katika moja ya instastories zake huku akisema kwamba sherehe hiyo ilikuwa inaanza saa moja usiku.

“Msichana wa saa. Hongera kwa kusherehekea kila baraka. Ninampenda sana msichana huyu. Anastahili haya na mengineyo!! Hongera sana msichana wangu Lulu kwa kupata ujauzito wake za kwanza,” Gloria Kyallo aliandika katika moja ya picha ya mbwa huyo aliyeuwa amemvalisha nguo kama mdoli vile.

Kama kawaida ya Wakenya, wengi walifurika kwenye upande wa kutoa maoni na kumuapiza kwa maneno makali huku wengine wakisema wanaelewa mapenzi ya mbwa ndio kama hivo na wengine wakisema hela kama hizo alizotumia kwa tafrija ya mbwa angezitumika kusaidia hata mtu mmoja anayeranda mitaani asiyekuwa na chakula wala pa kulala.

“Yaani mbwa anafanyiwa party Mimi hata keki sijaipata moja ikona jina langu,” mmoja kwa jina Ivy Leaky aliandika.

Huyu si mtu wa kwanza kuzushiwa kwa kusema anamthamini mbwa zaidi kuliko binadamu kwani wiki chache zilizopita mwanahabari maarufu kutoka Afrika Kusini, Moshe Ndiki alishangaza dunia baada ya kuandaa hafla ya mazishi ya kifahari kwa mbwa wake Sugar aliyefariki.

Katika mazishi hayo ambayo Ndiki alipakia video kwenye Instagram, watu walimzomea lakini akawajibu kwamba ni vizuri kila mtu kuyazingatia ya kwake na kuacha kupayukia mambo ambayo watu wanafanya na mali yao.