Anthony Hamilton azungumzia chakula alichokipenda akiwa Nairobi

Msanii huyo alisema anapenda sana kupika ila ndugu zake ndio wakosoaji na mashabiki wakubwa wa mapishi yake.

Muhtasari

• Hamilton alisema mara ya kwanza anapika Salmon na Spaghetti ilikuwa akiwa mjini New York ambapo walikuwa na marafiki wake 30 na walihisi njaa na hakuna aliyetaka kupika.

Msanii wa Soul kutoka Marekani, Anthony Hamilton awali katika mahojiano
Msanii wa Soul kutoka Marekani, Anthony Hamilton awali katika mahojiano
Image: Instagram//AnthonyHamiltonOfficial

Je, una mpango wa wikendi hii ama utakuwa unatebwereka tu nyumbani hali ya kuwa ni mwisho wa mwezi?

Kama huna habari basi za chini ya zulia ambazo zimewekwa mezani katika mitaa yote ya jiji la Nairobi ni ujio wa msanii maarufu kutokea Marekani ambaye ataziteka anga za jiji hili usiku wa tarehe 30 Julai hadi saa za majogoo, si mwingine bali ni Msanii nguli wa mitindo ya Soul na RnB, Athony Hamilton ambaye tayari ametua nchini tayari kwa hafla kubwa kubwa kabisa ya Stanbic Yetu ambayo itafanyika katika ukumbi wa Carnivore jijini Nairobi Wikendi hii ya mwisho wa mwezi.

Tulipata kuzungumza na msanii huyo alipotembelea studio za shirika la habari la Radio Africa Group, ambalo ndiye mshirika mkuu kwa kushirikiana na benki ya Stanbic ili kufaulisha tamasha hili kubwa ambalo halijawahi kutokea katika ardhi ya Kenya tangu mwaka huu kuanza.

Kukulia maisha katika eneo la Charlotte, jiji la Carolina Kaskazini, Marekani, mwimbaji aliyeshinda tuzo ya Grammy na gwiji wa muziki wa neo-soul Anthony Hamilton bila shaka ameyazuru maisha na sisi lengo letu lilikuwa kuyazamia zaidi maisha yake ya ndani, mbali kidogo na muziki. Tulitaka kujua ni vyakula vipi ambavyo anavishabikia zaidi.

Katika mahojiano, Mshindi huyo wa tuzo ya Grammy (ambaye pia ana uteuzi 16) alisema kwamba anajulikana kwa kuwashawishi watu wengi kwa sauti yake laini. Na marafiki zake, familia na wafanyakazi wa barabarani, kandi na muziki wanajua kuwa anaweza pia akakuchanganya na manukato ya uduvi wa kitunguu saumu, bata mzinga na vitoweo vya Salmon.

Hamilton alisema mara ya kwanza akiwa nchini Kenya mwaka 2014, alijaribu ugali na kusema kwamba alikipenda sana chakula hicho. Safari hii msanii huyo alisema kwamab alijaribu samaki, kuku na mahindi na ni chakula ambacho kilimpendeza ajabu.

"Leo nilikula samaki, kuku na pilau na nilifurahia sana," msanii huyo alielezea

Alisema kwamba akiwa Marekani anapenda Samaki aina ya Salmon ambayo alielezea mapenzi yake na chakula hicho pamoja na Spagjetti yalianzia wapi. Alisema wakati mmoja rafiki wake ambaye ndiye anamchezea gitaa la besi aliwahi mtembelea na akapata anapika Salmon pamoja na Spaghetti, alistaajabu sana ila alipoonja hakutaka tena kuachia.

“Rafiki yangu anayenichezea gitaa la besi Majibu yake ya kwanza alipoona upishi wangu yalikuwa, 'Je, unaweza kuweka Salmon ndani ya Spaghetti?' alipoonja sahani ilitoka kwenye chati!! Ilibidi asimame kwa dakika moja na akasimama kwa mshangao! alimpigia simu mke wake na kumwambia jinsi Spaghetti ya Salmon zilivyokuwa za kichaa. Alizungumza juu yake kwa siku kadhaa na kumwambia atengeneze. Bila shaka haikutoka vizuri kama yangu,” Hamilton alieleza.

Akielezea jinsi mapenzi yake kwa chakula hicho yalianza mpaka akakipenda na kuwa chakula anachokishabikia zaidi, Hamilton alisema kwamab alijipata tu kwani kipindi hicho hakuwa na chakula kingine, ila akafichua kwamba bado ana uwezo wa kupika vyakula vingine vingi.

“Nilijipata tu kwenye Spaghetti na Salmon. Sikuwa na chochote karibu nilipokuwa nikitengeneza Spaghetti…niliona Salmon aliyosalia na niliamua kupika Salmon. Wewe jaribu tu mambo, huwa najaribu vitu vipya wakati mwingine. Ninatengeneza kabichi nzuri sana, mbawa za bata mzinga, samaki wa bizari ya asali, vyote ni vizuri sana,” Hamilton alijigamba.

Tulitaka kubaini ni lini mara ya kwanza alijipata katika meko akifanya upishi na iwapo alipata ladha ile nzuri aliyokuwa akiikusudia mara ya kwanza alipoketi mekoni kujiandalia chakula alichokuwa akikifikiria na ladha aliyokuwa akiikusudia.

“Kweli ilikuwa wakati mmoja nilipokuwa katika eneo la New York/New Jersey na nilikuwa kwenye karamu ya nyumbani na watu 20 au 30. Kulikuwa na wanamuziki tofauti, wale wa kuchana mistari, waimbaji, na walinunua vyakula hivi vyote lakini hakuna mtu aliyejua kupika. Mimi na mvulana anayeitwa Gary tulianza kuweka kila kitu pamoja. Ilinibidi kufanya sufuria kubwa zaidi ya lasagna (anacheka). Nilioka na kukaanga vipande vingi vya kuku. Nadhani tulifanya sawa!” Hamilton alisimulia vile alivyojipata katika mkondo wa kupenda mapishi.

Hamilton alisema kwamba japo ulikuwa ni wakati mgumu wa kujipata katika kuanza kufanya jambo na mko kundi la watu kadhaa, ilibidi tu apike kwa sababu walikuwa njaa na walihitaji kutia kitu tumboni. Alisema kwamba hiyo ni talanta ya kiasili kwani hata mama na babake walikuwa wapishi Hodari Sana. Msanii huyo alidokeza kwamba kwake chakula ni kitu kingine chenye msisimuko mkubwa.

“Lazima uwe mahiri ama mwanamke au mwanamume kuweza kupika-kutikisa na kuoka na hayo yote. Kuna kitu cha kiroho kuhusu chakula kwangu. Tunaposema maneno, “Mungu nakushukuru kwa chakula hiki. Inashangaza. Kwangu, ni kama msisimko fulani. Chakula ni sehemu ya kipandisha hamu yangu katika kila jambo. Vionjo hivyo vinapokusanyika, rangi huchangamka….mwili huchangamka. Ninasisimka,” Hamilton alielezea mapenzi yake kwa chakula.

Alichekesha aliposema kwamba ndugu zake ndio wakosoaji wakubwa wa upishi wake ila akasema alimpikia mkewe kwa zaidi ya miaka kumi na alipenda sana mapishi yake.

“Ndugu zangu ndio wakosoaji wa upishi wangu. Wanalinganisha kila kitu na kupika kwa Mama yangu. Nina kaka wanne na dada mmoja. Ndugu zangu ndio wakosoaji wangu wakubwa, lakini wafuasi wangu wakubwa pia. Nilikuwa kwenye ndoa kwa muda mrefu. Yaani nilimpikia mke wangu kwa miaka 10. Sehemu kubwa ya kupika kwangu ilikuwa kwa ajili yake. Ikiwa utaweka upendo mwingi kwenye chakula, utapata majibu,” alisema gwiji huyo wa Soul.

Bila shaka mazungumzo yalikuwa mengi tena ya ucheshi kutoka kwa mkongwe huyu wa muziki wa Soul na R&B. itakumbukwa hii si mara yake ya kwanza kutua nchini kwani mara ya kwanza alikuwa humu ilikuwa ni mwaka 2014 wakati wa tamasha la Tusker Lite ambapo safari hii amekuja kwa ajili ya kutumbuiza kwenye tamasha la Stanbic Yetu, na hii itakuwa kubwa, si ya kukosa hii jamani!