Kwa nini Harmonize, Diamond na Alikiba wanatofautiana kimuziki?

Wasanii hao watatu ni maadui katika tasnia ya muziki huku ugomvi wa kutoka zamani ukiwa baina ya Diamond na Alikiba.

Muhtasari

• Ugomvi baina ya Diamond Platnumz na Alikiba umedumu kwa zaidi ya miaka 10 tangu wote wapate umaarufu.

• Harmonize ambaye aliletwa kweney umaarufu na Diamond kwa sasa anatajwa kuwa adui na tishio kubwa kwa msanii huyo.

Wasanii mahasimu wa bongo fleva, Harmonize, Diamond Platnumz na Alikiba
Wasanii mahasimu wa bongo fleva, Harmonize, Diamond Platnumz na Alikiba
Image: Instagram

Kwa muda kumekuwa na gumzo pevu kuhusu ni nani haswa mfalme wa miziki ya kizazi kipya ya Bongo baina ya bosi wa lebo ya Wasafi Diamond Platnumz na gwiji wa mashairi kutoka lebo ya Kings Music, Alikiba.

Watu mbalimbali wamekuwa wakiketi vijiweni kulijadili hili pasi na kuafikiana katika jawabu moja kwani kila mwamba ngoma siku zote huvuta upande wake.

Sasa mdau mmoja amejitokeza kuelezea tofauti kubwa baina ya wasanii hao wawili ambao wamehasimiana kwa zaidi ya mwongo mmoja tangu wapate umaarufu katika fani hii, cha kushangaza ni kwamba msanii bosi wa lebo ya Konde Music Worldwide, Harmonize amejipata katika Sakata hili ambapo pia ametajwa kuwa mmoja wa wasanii wanaolinganishwa sana na mahasimu hawa wawili wa tangu jadi.

Kulingana na mdau huyo mkereketwa na tasnia ya Bongo Fleva, tofauti baina ya Harmonize, Diamond Platnumz na Alikiba ni wazi na kubwa kuliko jinsi watu wanavyofikiria na hata kufanay kufuru ya kuwalinganisha katika viwango sawa.

Mdau huyo kwa jina Hopeman David anasema kwamba Alikiba ni msanii ambaye hapatawahi tokea kama yeye katika utunzi mzuri wa mashairi yaliyokwenda skuli, ila kilichomponza ni kwamba alishindwa kufanya muziki wake kuwa biashara, bali alilala sana katika kufanya muziki wake kuwafurahisha na kuwaburudisha mashabiki tu pasi na kujua kwamba muziki pia ni kazi na licha ya kuwa mtunzi mzuri, ipo haja ya kuufanya huo muziki kuwa biashara inayokuletea posho.

Kwa upande wa Diamond, mdau huyo anasema msanii Simba kinachomsaidia na kumweka kweney gemu mpaka sasa ni ujanja wake tu ,kwani msanii huyo anajua mbinu za kuufanya muziki wake upendwe hata kama hakuna cha muhimu anachokiimba. Anasema msanii Diamond anajua ujanja mwingi wa kuutangaza muziki wake kwa njia ya kibiashara kwa kuwekeza sana kwenye mapromosheni ya pesa nyingi kwa sababu anajua fika kwamba muziki kwake ni kama kazi na ambayo anaichukulia kwa umakini na uzingatifu mkubwa.

Harmonize ambaye anajipata katika viwango vya wawili hao ametajwa kuwa ni msanii aliyechipuka vizuri ila ametekwa na kiki. Harmonize anasemekana kuwekeza sana katika kiki, jambo ambalo wengi wanahisi litauponza muziki wake sana.