"Nilizimia na kupoteza fahamu saa 4, niliona mauti uso kwa uso" Owago Onyiro asimulia

Mchekeshaji huyo alidokeza kwamba siku tano zilizopita zilikuwa kama miaka kadhaa kwake baada ya kupoteza fahamu na nusra kufa.

Muhtasari

• "Niamini mimi sifi hivi karibuni tena kwa jina la Yesu..........Asante Bwana kwa kunifanya niishi tena,” Owago

Mchekeshaji Owago Onyiro
Mchekeshaji Owago Onyiro
Image: Instagram//OwagoOnyiro

Mchekeshaji Owago Onyiro amesema kwamba yuko hospitalini amelazwa kutokana na kile alisema kwamab alizimia kwa zaidi ya saa nne na alicheza shere na mauti.

Kupitia msururu wa picha alizopakia kwenye Instagram yake, Onyiro anasema kwamba alionana na Malaika Izraili, mtoa roho ana kwa ana na kumchezea shere kwani hakuweza kufanikiwa kumchukua. Alisema kwamba mahali alitoka baada ya kuzimia saa nne bila kujijua be wala te basi hawezi kufa hivi karibuni.

“Imeniwia shughuli nyingi kwa siku 4 zilizopita. Nilizimia na kupoteza fahamu kwa karibu masaa 4. Niliona mauti ya kweli na kurudi......... Niamini mimi sifi hivi karibuni tena kwa jina la Yesu..........Asante Bwana kwa kunifanya niishi tena,” Owago aliandika kwenye Instagram yake.

Katika picha nyingine akizingirwa na zaidi ya wahudumu wa afya watano, Owago Onyiro alisema kwamba alikuwa kidogo aipe dunia kisogo kabisa ila Mungu wa nafasi ya pili akamjaalia nafasi nyingine tena ya kuishi na kumshuru kwa maneno yaliyotukuka.

Alisema kwamba kwa sasa anaendelea kupata nafuu na kupakia picha akiwa karibu na bwagwa la kuogelea huku akidokeza kwamba ana upweke na ni kwa sababu watu wengi wanajifanya wanamjua kumbe kiuhalisia hawamjui hata chembe.

Muigizaji huyo ambaye pia ni mcheshi hakupata kudokeza hata kidogo kiini cha kupoteza fahamu kwa zaidi ya saa 4 kama alivyosema ila wachekeshaji na wasanii wenzake walifurika kwenye Instagram yake kumpa pole na kumtakia afueni ya haraka.

Wengine walisema kwamba kulazwa huko kwake hospitalini si tukio la hivi karibuni bali ni la kitambo kidogo huku wengine wakizidi kumtakia kupona kwa haraka.

Bado haijajulikana kama Owago Onyiro ni hivi majuzi amepatwa na hilo tatizo la kuzimia saa nne mfululizo bila kujitambua ama ni tukio la nyuma.