Eric Omondi Amewasuta Wasanii Kenya Kulala Mpaka Diamond Kuchukua Nafasi Yao

Wasanii mbalimbali wa humu nchini wameonesha kutoridhishwa kwao na hatua ya Raila kumleta Diamond kutumbuiza Kasarani.

Muhtasari

• "Kama Wanamuziki wetu hawatajitokeze na kuchukua nafasi zao, hii itazidi kuwa mbaya" - Eric Omondi.

• "Nasubiri tu vikao vya BUNGE virudi nitafanya sehemu yangu na kuhakikisha tunapita 75% PlayKE" - Eric alisema.

Msanii Diamond Platnumz na EQRIC Omondi
Msanii Diamond Platnumz na EQRIC Omondi
Image: Instagram

Msanii na mchekeshaji namba moja Afrika kwa muda wote Eric Omondi amepata kutilia neno lake matukio yaliyotokea humu nchini katika uwanja wa Kasarani ambapo msanii kutoka Tanzania Diamond Platnumz alitumbuiza katika hafla ya mwisho ya mkutano wa kisiasa wa Azimio la Umoja One Kenya.

Eric Omondi ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipigana kwa udi na uvumba kutetea muziki wa humu nchini huku akitamba taasisi zote na washikadau kukumbatia kucheza miziki ya Kenya kwa asilimia 75, alisema kwamba hana ubaya na Diamond Platnumz ila inasikitisha sana kwamba katika halfa ya kihistoria kama ile ya Kasarani, hakuna msanii hata mmoja wa humu nchini alipata kutambulika na kuoenekana kuwa wa thamani.

“Ni siku ya huzuni sana kwa Tasnia ya Muziki wa Kenya. Kwanza kabisa niMPONGEZE ndugu yangu @diamondplatnumz kwa Kuendelea Kuinua Bendera ya Afrika Mashariki. Hongera kaka!!! Pili inasema mengi kwamba kwa wakati huu WA UHAKIKA na WA KIHISTORIA katika Taifa letu, hakuna hata mwanamuziki wetu wa humu nchini alionekana kuwa wa thamani na kustahili!!!” Eric Omondi alionyesha kutoridhishwa kwake.

Mchekeshaji huyo alionekana kuwalaumu wasanii kwa kutojijenga vizuri na kujikuza kwa njia inayoweza kuwapeleka kwenye majukwaa makubwa na ya kihistoria kama hayo.

Msanii huyo alisema wasanii wa humu nchini walikataa kumsikiliza na hata kumuunga mkono wakati alisimama kupigania haki ya 75% ya muziki wa humu nchini kupewa kibao mbele.

“Simlaumu yeyote ila Wanamuziki!!! Kama Wanamuziki wetu hawatajitokeze na kuchukua nafasi zao, hii itazidi kuwa mbaya!!! NISIKILIZE!!!! Nimesema haya na nitayasema tena. PIGA KAZI!!! Tunahitaji SHOWBIZ!!! Sio haya mambo ya KUCHOSHA, YA KUTABIRIWA na YA KUTUMIWA mnayoendelea kutudunda!!! AMKA!!!! AMKA!!! Nasubiri tu vikao vya BUNGE virudi nitafanya sehemu yangu na kuhakikisha tunapita 75% PlayKE lakini LAZIMA MUAMKE!!! NIMEMALIZA!!!” Eric Omondi aling’aka.

Eric Omondi kwa kipindi kimoja katika moja ya mitikasi yake alifanya kufuru ya kuandamana nje ya bunge la kitaifa akiwataka wabunge wamsikilize na kupitisha mswada wa kuweka kuwa sheria miziki ya humu nchini kupewa kipaumbele kwa 75%. Omondi alidundwa na maafisa walinda usalama lakini pia hakuchoka, baade tena alirudi pale kwa amani akiwa ndani ya kijigari cha vioo alichojifungia ndani huku akiahidi kutorudi nyumbani mpaka wabunge wamsikilize.

Baadhi ya wabunge walijitokeza na kumsikiliza na hata kumuahidi kuendelea na mswada huo bungeni utakaopitisha sheria kwa vyombo vya habari humu nchini kucheza muziki wa Kenya kwa asilimia 75 ya miziki yote kila siku.

Wasanii wengine ambao wamesuta tumbuizo la Diamond ni Juliani ambaye aliandika kwenye instastory yake akisema kwamba ni makosa na aibu kwa msanii huyo kutumbuiza kweney hafla ya wakenya hali ya kuwa nchini Kuna wasanii wa kutosha tena wenye talanta kubwa.