"Private Jet Inakuja Pia!" Baba Levo Adokeza Baada ya Diamond Kununua Helikopta

“Hii helcopter haipo eastafrica labda kwenye majeshi tu - Baba Levo aliisifia.

Muhtasari

• "Helcopter imeshafika tanzania tayari. Ndege ya kibinafsi inakuja pia..!” aliandika Baba Levo.

Msanii Diamond Platnumz akitangaza kununua ndege yake
Msanii Diamond Platnumz akitangaza kununua ndege yake
Image: Instagram//DiamondPlatnumz

Msanii Diamond Platnumz ametangaza kununua ndege yake aina ya helikopita hatimaye, siku kadhaa baada ya uvumi kuzuka kuhusu uwezekano wake kumiliki ndege.

Msanii huyo nambari moja kwa muda wote kwenye ukanda wa Afrika Mashariki alitangaza habari hizo njema kupitia instastory yake akimshukuru Mungu kwamba hatimaye amefanikiwa kununua ndege aina ya helikopta.

“Mungu ni mwema, nimenunua helikopta yangu leo,” aliandika Diamond.

Maneno haya ya Diamond yanakuja siku chache tu baada ya chawa wake fundi majumba Baba Levo kutangaza kiutani kwamba Diamond anamiliki ndege lakini kama kawaida watu wakampuuza kwa kusema kwamba hiyo ni tabia yake ya uchawa na kutaka muda wote kujipendekeza kwa Diamond ambaye katika wakati mmoja alisema ndiye alimleta kweney uso wa umaarufu mitandaoni na hata kufanya muziki huku pia akifanya kama mtangazaji wa zamu katika stesheni ya Diamond Platnumz, Wasafi.

Baba Levo kwenye ukurasa wake wa Instagram alisema kwamba huo si mwisho wa Diamond kwani bado ndege ya kibinafsi ipo njiani na inakuja hivi karibuni tu na ni suala la Subira tu kwa mashabiki wa Simba kudhibitishiwa hilo pia.

“Haya niliwaambia mkanitukana tajiri kaandika mwenyewe..!!! Helcopter imeshafika tanzania tayari. Ndege ya kibinafsi inakuja pia..!” aliandika Baba Levo.

Baba Levo alizidi kutolea sifa za helikopita hiyo huku akisema ina uwezo wa kusafiri muda wote na pia kuwa na uwezo wa kipekee katika mambo mbalimbali.

“Hii helcopter haipo eastafrica labda kwenye majeshi tu..!! Sifa zake ni hizi; inaweza kusafiri usiku na mchana, ina injini mbili, inapakia watu nane kwa pamoja, inauwezo wa kupambana na hali ya hewa yoyote hata kama ni mbaya kiasi gani..!! Mfano mvua kali, au joto kali au ukungu, ina matenki makubwa ya mafuta, inaweza kutumika kwenye kuokoa watu kwenye majanga au kuzima majanga ya moto uakitokea, kasi ni balaaa, shikamooo boss @diamondplatnumz ..!!,” Baba Levo alisema.