Sean Andrew apakia video ya zamani babu yake Kibaki akisisitiza Amani

Sean Andrew ni mjukuu wa hayati Mwai Kibaki mwenye umaarufu mkubwa Instagram.

Muhtasari

• "Haina haja kumuita mtu majina kwa sababu ana haki ya kutoa maoni." - Kibaki.

Mjukuu wa Mwai Kibaki Sean Andrew awasihi wakenya kudumisha amani
Mjukuu wa Mwai Kibaki Sean Andrew awasihi wakenya kudumisha amani
Image: Instagram//SeanAndrew

Mjukuu wa Mwai Kibaki Sean Andrew amepakia mkanda wa video kwenye instastories zake ambao ni wa marehemu babu yake Rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki akiwataka wakenya kuvumiliana haswa kipindi hiki ambapo nchi inajiandaa kutangaziwa rais mpya na viongozi wngine katika nyadhifa zingine tano.

Katika mkanda huo wa video unaomuonyesha Mwai Kibaki enzi za ujana wake, anasikika akiwarai Wakenya kukumbatia amani na kuvumiliana kwa hisia na maoni ya kila mmoja kwani nchi haiwezi kusonga mbele kama watu watatofautiana kisiasa mpaka kufikia kiwango cha kuzushiana fujo.

“Nataka kuwaambia Wakenya kuwa wavumilivu kwa sababu demokrasia haiwezi kudumu kama hatutavumiliana, unamvumilia rafiki yako, Jirani yako na kuwaacha wawe na maoni tofauti na yako, haina haja kumuita mtu majina kwa sababu ana haki ya kutoa maoni. Hiyo ni haki yake ya kimsingi na hakutengenezwa ili kutawalwa kimaoni na wewe wala kuongozwa na wewe” Kibaki anaonekana akizungumza kwenye video hiyo ya kitambo kiasi.

Sean Andrew alizidi mbele kuonesha dhibitisho kwamba alipiga kura yake katika eneo bunge la Westlands Nairobi na kuwasihi wakenya wote mashabiki wake kudumisha amani muda wote.

Andrew ni mjukuu wa rais hayati Mwai Kibaki na alikuwa na ukaribu mkubwa sana na babu yake huyo ambaye wakati wa kifo chake alionekana kudhoofika mno.

Aliivua moja ya pete zake na kuirusha kaburini mwake kama ishara moja ya kumuenzi kwa mapenzi ya dhati kama babu mwema.

Rais Kibaki alihudumu kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2013 kama rais wa tatu wa Kenya kabla ya kustaafu.