(+video)Jinsi Sammy Brayo, Jamaa asiye na Mikono na Mguu uliolemaa alipiga Kura

Brayo ni mlemavu mwenye umaarufu kwa weledi wa kucheza piano bila mikono.

Muhtasari

“Nilishiriki leo katika kupiga kura kama mpiga kura kwa mara ya kwanza - Sammy Brayo.

Sammy Brayo, kijana mwenye ushawishi mkubwa kwenye mtandao wa Instagram kutokana na ulemavu wake wa kukosa mikono yote na mguu mmoja kulemaa amepakia video akionesha furaha yake baada ya kupiga kura kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yake.

Brayo alijizoea umaarufu kutokana na weledi wake wa kucheza Piano kwa kutumia mguu wake mmoja uliolemaa ambao umelegea kama mkono na pia kufanya shughuli zingine kama kawaida licha ya kutokuwa na mikono yote pamoja na mguu mmoja kuwa na ulemavu.

Alipakia video hiyo huku akidokeza kwamba ulemavu wake haukumzuia kushiriki katika kutimiza wajibu wake wa kidemokrasia kuwachagua viongozi wake na pia kusema kwamba alirauka alfajiri Jumanne Agosti 9 kwa ajili hiyo kwani ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki uchaguzi.

“Nilishiriki leo katika kupiga kura kama mpiga kura kwa mara ya kwanza. Watu tulirauka,tushatoka katika kituo,” alishirikisha video hiyo kwa haya maneno.

Mashabiki wake walimshabikia na kumsherehekea kwa hitimo kubwa ambalo anazidi kuonesha watu wenye ulemavu kwamba hali hiyo ya kimaumbile si mwisho wa maisha bali watu kama hao pia wana uwezo wa kufanya kitu chochote watakacho wakijiamini na kujituma zaidi kwani wamebarikiwa kwa njia ya kipekee.

“Unanionyeshea kuna SABABU MILIONI ZA Kuishi. Kila muda nikiona Video yako hapa Instagram lazima nipunguze kasi na niLike,” Mmoja aliandika.

“Nimefurahishwa sana Sammy Brayo. Wewe ni Mkenya mzalendo, tunaomba na kutumai Kenya yenye amani,” Shabiki mwingine pia alimshabikia.

Wakenya wa matabaka mbalimbali walijitokeza kwa wingi Jumanne kushiriki katika mchakato huo wa kutimiza wajibu wao wa kidemokrasia kwa kuwachagua viongozi wao katika nyadhifa sita tofauti.