Mamake Diamond amsherehekea mpenziwe, Uncle Shamte kwa ujumbe wa kimahaba

Uncle Shamte ni mpenzi wa mamake Diamond

Muhtasari

• Mamake Diamond mara kadhaa ameyadhihirisha mapenzi yake kwa mwanaume huyo wazi bila haya licha ya kuwa na watoto wakubwa kama kina Diamond, Romyjones na dadake Esma.

Uncle Shamte na mpenzi wake Mama Dangote
Uncle Shamte na mpenzi wake Mama Dangote
Image: Instaram//Uncle Shamte

Sandra, au Mama Dangote kama wengi wanavyomjua kupitia mitandao ya kijamii ni mamake msanii nambari moja wa muda wote katika ukanda wa Afrika mashariki, Diamond Platnumz.

Ijumaa ilikuwa siku ya kuzaliwa ya mpenzi wake wa ubani Uncle Shamte na Mama Dangote hakusalia kimya kwani alichukua katika ukurasa wake wa Instagram na kuachia ujumbe mzuri wa makopa kopa kwa Shamte akimtakia kila la kheri katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Mamake Diamond alimpamba kwa maneno ya kudondosha denda mwanaume huyo wake kwa kumuita rafiki yake wa karibu na pia kipenzi chake.

Kikubwa alichomtakia ni kuwa na maisha marefu katika ramani ya dunia hii ili wazidi kugandana pamoja mithili ya tumbili kwenye mgomba wa ndizi katika bahari ya mapenzi isiyojua kiangazi.

“Leo kazaliwa rafiki yangu kipenzi Mume wangu.. Maisala Abdu Shamte...Nakutakia maisha marefu yenye baraka tele @uncle_shamte Baba muuza viwanja..” Mama Dangote aliandika.

Kwa familia ya kina Diamond na nduguye Esma na Romyjons, Uncle Shamte anasimama kama baba wa kambo kwani mahusiano yake na Mama Dangote hayana muda mrefu tangu walipoanza.

Diamond amekuwa akisemwa mitandaoni kwamba hajawahi kumsaidia babake wa kumzaa licha ya picha kusambazwa mitandaoni kuonesha hali yake duni akivaa matambara.

Mama Dangote naye alisherehekea siku yake ya kuzaliwa miezi michache iliyopita ambapo Diamond alimtunuku zawadi ya shilingi milioni 20 za Kitanzania na sasa wengi wanasubiri kuona ni zawadi gani msanii huyo anayenukia mihela atampa babake wa kambo kama kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa.