Octopizzo amtaka rais mteule Ruto kuhalalisha bangi

Msanii huyo alisema suala la bangi ndilo lilifanya wengi kumshabikia Wajackoyah

Muhtasari

• “Najua wewe ni mkristo na kwa hiyo hili gumzo huenda litakuwa gumu kidogo kwako lakini unajua bangi ni moja ya dawa ambazo ni takatifu zaidi duniani." - Octopizzo

Msanii huyo amemrai rais mteule kuhalalisha bangi
Ruto, Octopizzo Msanii huyo amemrai rais mteule kuhalalisha bangi
Image: Facebook, Instagram

Mwanamuziki wa kuchana mistari Octopizzo amemtaka rais mteule William Ruto kuihalalisha bangi pindi tu atakapokula kiapo cha kuingia ofisini kama rais wa tano wa Kenya.

Katika video ambayo imesambazwa mitandaoni, Octopizzo anamuelezea Ruto kwamba hata kama ataona kuhalalisha bangi ni jambo gumu basi aifanye isiwe kama ni hatia kwa mtu anayepatikana naye bali liwe tu ni jambo la kawaida.

“Najua wewe ni mkristo na kwa hiyo hili gumzo huenda litakuwa gumu kidogo kwako lakini unajua bangi ni moja ya dawa ambazo ni takatifu zaidi duniani. Na amabcho nakuomba hata si kuhalalisha matumizi yake bali ni kuiweka bangi isiwe kama hatia kwa mtu anayepatikana nayo,” Octopizzo alihoji.

Octopizzo akizungumzia mkutano wa hivi majuzi ambao Ruto alishiriki na wajumbe wa amani waliotumwa kutoka Marekani kuzungumza na viongozi wakuu nchini ili kuhubiri amani, alisema kwamab Ruto alikutana na seneta wa Delaware na kusema kwamba huko katika jimbo la Delaware mtu anaruhusiwa kutembea na bangi mradi tu amehitimu umri wa miaka 21 kwenda juu.

“Juzi nilikuona ulikutana na seneta wa Delaware, huko mtu anaruhusiwa kutembea na bangi gramu 3 kwa kujivinjari tu ilmradi mtu ako na miaka 21. Hii ni biashara ya mabilioni na tunajua kuna watu serikalini wenye wanafanya biashara hiyo,” Staa huyo wa hiphop alisema.

Alizidi kufafanua kwamba bangi kufanywa kuwa ni hatia kwa mtu anayepatikana nayo kumewaweka vijana wengi gerezani ambapo alisema amefanya kazi na gereza la Kamiti na ameona vijana wengi wamehukumiwa kwa kosa la kupatikana na bangi yenye thamani ya shilingi mia, jambo ambapo alilitaja kuwa si haki kabisa kwa vijana hao.

Kulingana naye katika video hiyo, Octopizzo anasema kwamba kama mtu anafanya magendo ya kuuza bangi kilo kadhaa ndio anafaa kuchukuliwa hatua lakini kwa mtu anayepatikana na msokoto mmoja tu si vyema kufungwa jela kwa sababu wengi wao wanatumia bangi tu kama njia moja ya kuwaepushia msongo wa mawazo.