Elon Musk: Kupungua kwa idadi ya watu wanaozaliwa ni athari kubwa kuliko 'global warming'

Musk aliwataka watu kukumbatia mfumo wa kuzaana kwa wingi ili kukuza ustaarabu wa dunia.

Muhtasari

• Musk aliwataka watu kukumbatia mfumo wa kuzaana kwa wingi ili kukuza ustaarabu wa dunia.

• Anasema dunia itapata changamoto zaidi kuliko ile ya tabia ya nchi endapo watu watazidi kupungua kuzaliwa.

Tajiri namba moja duniani awataka watu wazaane kwa wingi
ELON MUSK Tajiri namba moja duniani awataka watu wazaane kwa wingi
Image: MAKTABA

Tajiri namba moja duniani mwenye utata mkubwa kutokana na kauli zake zisizoeleweka mbele nyuma kama kitumbua, Elon Musk kwa mara nyingine tena amezua mjadala mkali kwenye mtandao wa Twitter.

Elon Musk bila kutetereka asubuhi ya Ijumaa alitoa msimamo wake kwa kusema kwamba watu kuwa wazembe katika uzazi na kutozaa watoto wengi ni athari kubwa katika ulimwengu kuliku athari za tabia ya nchi kwa kimombo ‘global warming’

Musk anasema kwamab watu wengi wanaamini athari za tabia ya nchi ndiyo athari kubwa kabisa itakayokumba mataifa mengi katika miaka michache ijayo lakini amelipinga hilo kwa kusema kwamba watu kutozaana ndilo litakuwa tatizo kubwa haswa!

“Kuporomoka kwa idadi ya watu kutokana na viwango vya chini vya kuzaliwa ni athari kubwa zaidi kwa ustaarabu kuliko ongezeko la joto duniani na tabia ya nchi, zingatia maneno haya yangu,” Musk alisema.

Watu wengi duniani wamekumbatia mfumo wa uzazi wa mpango ili kujaribu kudhibiti idadi ya watoto wanaozaliwa kutokana na hali ya uchumi kuzorota na gharama ya maisha kupanda kila uchao.

Wengi walipinga vikali kauli hii ya Musk ya kuwataka watu kuzaana kwa wingi ili uepusha kile alichokiita athari ya kutokomea kwa ustaarabu kutokana na idadi ndogo ya watu wanaozaliwa na wengi wakizidi kutangulia mbele za haki.

“Je, kuwa na watoto ndio suluhisho pekee? Nadhani kuna haja ya kuwa na Elimu ya kutosha juu ya suala hili,” mmoja alisema.

“Kuna tofauti kati ya kiwango cha kuzaliwa na idadi ya watu. Kiwango cha kuzaliwa kinapungua katika maeneo mengi. Katika miongo kadhaa, tutaona idadi ya watu ikipungua kwa kiwango cha kuzaliwa kilichopo,” mwingine aliongezea.