Nilikuwa nafika shughulini kwa miguu, sasa natua kwa helikopta - Moya David

Wiki jana alikuwa Dubai katika tafjia Iliyofanyika ndani ya boti aina ya Yatch

Muhtasari

“Usifanye kazi kwa ajili ya kutambuliwa bali fanya kazi inayostahili kutambuliwa." - Moya David.

Mcheza densi
Moya David Mcheza densi
Image: INSTAGRAM

Mcheza densi maarufu kwa kuwashtukizia watu katika hafla mbali mbali Moya David amezungumzia hatua zake katika maisha ambapo amechukua fursa hiyo kuwahimiza na kuwamotisha watu wanaoanza kwamba juhudi ndio siri ya mafanikio katika kila kitu unachokifanya.

Kupitia Instagram yake, David alipakia msururu wa picha akiwa kando ya ndege aina ya helikopta ya kijani na kusema kwamba safari ya mafanikio yake ilianza wakati alikuwa anatembea kuwashtukizia watu kwa miguu ila siku hizi anatua kwenye mitikasi kama hiyo kwa ndege.

Aliwashauri mashabiki wake kutojikita katika kutaka kujulikana tu bure bali kushiriki katika kuvifanya vitu ambavyo vitawafanya wajulikane.

“Usifanye kazi kwa ajili ya kutambuliwa bali fanya kazi inayostahili kutambuliwa. Kutoka kutembea hadi kwa watu na kushtukiza hadi sasa kutua kwa helikopta kwa kazi hiyo hiyo! Siku zote ninashukuru Mungu na nyinyi mashabiki wangu!” Moya David alisema.

Hivi majuzi, mcheza densi huyo alitangaza kufungua kinyozi chake cha kifahari katika mtaa wa kifahari wa Kilimani kutokana na mapato ambayo amekuwa akipokea kutoka kwa kazi yake ya kushtukiza kwa watu na kuwachezea densi kwa sekunde kadhaa.

Safari yake ya kwanza kwa kutumia ndege katika shughuli hizo ilikuwa ile ya kuelekea kisiwa kimoja bahari hindi ili kucheza densi kwa ziara ya wanandoa wa bonfire adventures, Sarah Kabu na mumewe Simon Kabu.

Juzi kati pia alipakia picha na video akiwa Dubai kushiriki katika tafrija kwenye mtumbwi aina ya Yatch ambapo alienda kuwashtukiza kwa kucheza densi watu kwa mwaliko rasmi wa malipo.