Kwa nini mpiga picha wa Diamond alipost Harmonize na kumuita Kipenzi cha Bosi?

Lukamba alikuwa mpiga picha rasmi wa Diamond kabla ya wiki chache zilizopita kugura WCB Wasafi.

Muhtasari

• Kauli ya kumuita Harmonize kipenzi cha bosi kilizua mkanganyiko mitandaoni baadhi wakidai bosi anayezungumziwa ni Diamond Platnumz.

• Ikumbukwe kipindi fulani Diamond aliwahi kiri kwamba Harmonize ndiye msanii aliyekuwa na riziki kubwa kipindi akiwa Wasafi.

Mpiga Picha wa Diamond Platnumz Likamba apakia picha ya Harmonize
Mpiga Picha wa Diamond Platnumz Likamba apakia picha ya Harmonize
Image: INSTAGRAM

Wiki ziliyopita, palizuka taarifa zisizo za kufurahisha mashabiki wa WCB Wasafi baada ya mpiga picha rasmi wa msanii Diamond Platnumz, Lukamba kutangaza kujiachia kutoka rekodi lebo hiyo na uhusiano na msanii huyo.

Mpiga picha huyo sasa amezua utata mkubwa kwenye ukurasa wake wa Instagram baada ya kuendeleza msururu wa kupakia picha za wasanii waliotangulia kuigura WCB wakiwemo Rich Mavoko, Harmonize na Rayvanny huku katika kila kapsheni akifuatisha na maneno ya ‘Saa kumi na mbili jioni’

Hili limezua gumzo kubwa sana wengi wakijiuliza ni nini hiki ambacho anacho na wasanii hao na tukio ambalo limezua gumzo la mkanganyiko hata zaidi ni pale alifuatisha picha ya msanii Harmonize kwa kusema kwamba ni ‘Kipenzi cha Bosi’

Gumzo kubwa lilijikita kwenye picha hiyo ya Harmonize huku baadhi wakimsuta kwamba pengine baada ya kuvunja uswahiba wake na Diamond Platnumz sasa ameungana mikono na Harmonize ambaye licha ya kuwa Diamond ndiye alimuinua na kumleta kweney mwanga wa Bongo fleva ila kwa sasa ni mahasimu wakubwa sana wasioweza kupikika katika chungu kimoja.

Wengi wakirejelea kapsheni ile ya ‘Kipenzi cha Bosi’ walianza kuchanganua na kutaka kubaini bosi anayezungumziwa hap ani nani labda. Wengine walikisia kwamab bosi ni Diamond Platnumz na sasa ni kwa nini labda Lukamba amwite Harmonize kama ni kipenzi cha Diamond, kama kweli yeye ndiye bosi anayezungumziwa hapa?

Itakumbukwa miaka kadhaa nyuma baada ya Harmonize kuondoka WCB kwa utashi mno, alianza kumchimba mikwara bosi wake Diamond na kutoa ufichuzi mkubwa ambao uliambatana na jinsi alikuwa ananyonywa na kukandamizwa chini ya lebo ya WCB.

Diamond ambaye wengi wanamjua si muongeaji sana haswa ikija ni masuala ya kujibu maneno yanayohusu tuhuma za lebo yake, katika kipindi kimoja alinukuliwa akisema kwamab katika watu ambao alikuwa anawathamini sana na ambao walikuwa na riziki kubwa ndani ya Wasafi ni msanii Harmonize.

Sasa kauli hii imeambatanishwa na maneno hayo ya Lukamba kumuita Harmonize kipenzi cha bosi na wengi wameweza kusema kwamba huenda bado Diamond anamkubali sana Harmonize kwa kuzidi kuipeperusha bendera ya muziki wa bongo licha ya kila mmoja kuwa na timu yake.

Diamond katika mahojiano na kituo cha DW huko Ujerumani wiki chache zilizopita, alinukuliwa akisema kwamba akiona wasanii aliowashika mkono wanainuka basi huwa na furaha kubwa kama baba aonapo watoto wake wanafanikiwa.