Uliona venye Nilishughulika na nyinyi Mombasa - Babu Owino amtania Jaguar

Kila mahali tuliwafukuza - Owino alimtania Jaguar.

Muhtasari

• Jaguar alikuwa amepakia picha zake akizungumzia maudhui mbali kabisa na siasa.

• Babu owino alifika pale na kumkumbusha kwa njia ya utani jinsi UDA ilivyobwagwa ugavana Mombasa na ODM.

Mbunge Babu Owino amtania Jaguar kuhusu UDA kushindwa Mombasa na ODM
Mbunge Babu Owino amtania Jaguar kuhusu UDA kushindwa Mombasa na ODM
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino baada ya ODM kushinda ugavana Mombasa ambapo alikuwa mmoja wa waangalizi wa uchaguzi ule, hajamaliza kusherehekea huku akiwakejeli wenzake kutoka Kenya Kwanza.

Owino ambaye anajulikana kwa mitikasi yake ya kutema maneno hovyo kwenye mitandao ya kijamii, safari hii alitua kwenye ukurasa wa Facebook wa aliyekuwa mbunge wa Starehe, Charles Njagua.

Njagua ambaye wengi wanamjua kwa jina lake la usanii kama Jaguar alipoteza katika kura ya mchujo wa UDA alikokuwa analenga tikiti hiyo kutetea kiti chake.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, alipakia picha zake mbili na kusema tu kwamba ‘Jichaji mwenyewe’ bila kugusia suala lolote la kisiasa. Lakini kwa Babu Owino, hii ilikuwa nafasi nzuri ya kumtupia kejeli kumkumbusha jinsi Azimio ilichachafya Kenya Kwanza kwenye kipute cha ugavana Mombasa.

Babu Owino alimtabia kwamba Mombasa ambako alikuwa mwangalizi mkuu kwa upande wa Azimio la Umoja One Kenya, aliwaonesha kivumbi wabunge kadhaa wa Kenya Kwanza waliokuwemo kufanya uangalizi wa kura.

“Uliona venye Nilishughulika na nyinyi Mombasa, mwanaume mmoja ndigi yenu wabune 90 kutoka Kenya Kwanza. Hata hamngeweza kufanya kitu chochote. Kila mahali tuliwafukuza,” Babu Owino alimkumbusha.

Owino alikuwa akiangalia na kulinda kura za mgombea wa tikiti ya ODM Abdulswamad Shariff Nassir ambaye alikuwa akimenyana na Hassan Omar Sarai wa UDA.

Abdulswamad Nassir alishinda kiti cha ugavana Mombasa baada ya kupata kura 119,083 katika uchaguzi huo uliocheleweshwa na IEBC baada ya kuwepo mkanganyiko katika usambazaji wa karatasi za kura Agosti 9. Mpinzani wake mkuu, Hassan Omar wa UDA aliibuka wa pili baada ya kupata kura 98, 108.

Pia kule Kakamega jeshi la Odinga likiongozwa na gavana mteule wa Kisii, Simba Arati walikita kambi katika vituo mbali mbali kufanya uangalizi wa kura za mgombea wa ODM Fernandes Barasa aliyekuwa akiwania dhidi ya seneta aliyeondoka Cleophas Malala wa ANC. Barasa aliibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Odinga alifurahikia matokeo hayo huku akiwasifu Nassir na Barasa kwamba sasa kenya mzima inaweza ikajua kwamba kweli Azimio la Umoja One Kenya ni wimbi lisiloweza kudhibitiwa.