(+video) Baada ya kimya cha muda, Diana Marua aibuka na ujauzito uliokomaa

Miezi kadhaa iliyopita wanandoa hao waliweka wazi kuhusu kutarajia mtoto wao wa tatu pamoja.

Muhtasari

• Siwezi kusubiri kukutana nawe, kukushika na kukuinua kuwa Mfalme/Malkia wangu - Diana Marua

Baada ya kupoteza katika kinyang’anyiro cha ubunge Mathare, Bahati anatarajia kurudisha tabasamu kwenye uso wake kwa kumpokea mtoto wake hivi karibuni.

Haya yanadhihirika bayana kutokana na video ya mkewe Diana Bahati ambayo aliipakia kwenye Instagram yake akionesha ujauzito wake uliokuwa mkubwa kabisa, jambo ambalo liliwafanya mashabiki wa wanandoa hao kukisia kwamba baraka hiyo inatarajiwa kudhihirika siku si nyingi kutoka sasa.

Msanii Bahati ambaye tangu kukamilika kwa uchaguzi huo ambao alibwagwa kwa mbaaali hadi nafasi ya tatu kwa kura elfu nane na ushee hivi hajawahi kuzungumzia kilichojiri, wiki tatu sasa tangu mshindi kutangazwa na kukabidhiwa cheti na IEBC na hata kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii amekuwa ni mchache mno kupakia vitu kama ambavyo ilikuwa kawaida yake hapo awali.

Mara ya mwisho akipakia kwenye Instagram yake ikiwa ni ile alikuwa anajitanua kifua kwamba alitumia zaidi ya milioni 33 za Kenya kwenye kampeni na siku ya ndovu kumla mwanawe ambayo ilikuwa siku ya uchaguzi alidhamiria kumwaga shilingi milioni 10 ili kumaliza kwa kishindo kama mwanariadha kwenye mkumbo wa mwisho.

Wanafamilia hao baada ya kimya hichi chao, sasa Diana Marua amekuja upya huku akiwasha mitandao na video nzuri inayoonesha ujauzito uliokomaa ambao wengi wamekisia uko katika duru ya mwisho kabisa kabla ya mtoto kuzaliwa.

Marua baada ya kupakia video hiyo akijisogeza kitaratibu na ujauzito wake, aliifuatisha kwa kusema kwamba alikuwa amewapeza sana mashabiki wake kwa kuwarushia kitu cha kuwafanay wazidi kumzungumzia.

Alidokeza kwamba tangu kugundua ana ujauzito wa wiki nane mpaka sasa, ameendelea kuhisi kuongezeka kwa upendo kwa kiumbe hicho ambacho amekibeba tumboni.

“Je, unaundaje uhusiano wa kina na moyo ambao hujawahi kukutana nao? Kuanzia wiki 8 mpaka sasa, nimekua nikikupenda... Pamoja na yote niliyo nayo, nitakupenda mpaka mwisho wangu. Siwezi kusubiri kukutana nawe, kukushika na kukuinua kuwa Mfalme/Malkia wangu milele,” aliandika Diana Marua.