"Ukicheza kama wewe utakuwa rais ajaye" Nameless amwambia Sakaja

Sakaja alichaguliwa kama gavana wa Nairobi kupitia chama cha UDA na kuapishwa kama gavana wa nne.

Muhtasari

• “Kaka.. ukicheza hii kitu vizuri wewe ni rais ajaye kimchezo!! Cheza kama wewe! Cheza vizuri. Kila la kheri!” Nameless alimuandikia Sakaja.

nameless
nameless

Mwanamuziki wa muda mrefu, Nameless ameonekana kufurahishwa na kutiwa motisha na hatua za gavana mpya wa Nairobi, Johnson Sakaja katika kitivo cha siasa za humu nchini.

Juzi kati gavana Sakaja alipakia picha kweney ukurasa wake wa Facebook akidokeza kwamba rasmi safari ya utawala wake Nairobi imeng’oa nanga. Alikuwa amejumuika kwenye mkutano na wafanyikazi wa jiji wakiweka mipango jinsi watakavyotekeleza masuala mbalimbali kwa wana Nairobi.

“Mwanzo mzuri na wafanyikazi wetu wa kaunti asubuhi ya leo. Tumesikiliza na tumetiwa moyo kwamba azimio na malipo ni wazi. Mji wa utaratibu na heshima; matumaini na fursa kwa wote. Twende Kazi,” Sakaja aliandika kwenye ukurasa wake.

Nameless alikuwa miongoni mwa wakaaji wa Nairobi waliofurika kwenye sehemu ya kutolea maoni na kumuonea Fahari Sakaja kwa kumtakia kila la kheri katika safari ya utawala wake kama gavana.

Alimuambia kwamba akijinafasi vizuri kwa kuwafanyia watu wa Nairobi kazi basi kazi yake itampa umaarufu mkubwa kote nchini. Alisema huenda utendakazi wake Nairobi ukiwa mzuri atatunukiwa kiti cha urais na wananchi.

“Kaka.. ukicheza hii kitu vizuri wewe ni rais ajaye kimchezo!! Cheza kama wewe! Cheza vizuri. Kila la kheri!” Nameless alimuandikia Sakaja.

Gavana Sakaja amekuwa akishabikiwa na wengi huku wakiwa na matumaini sufufu kwamba jiji la Nairobi huenda tayari limepata tiba halisi kwa masaibu chungu nzima yanayokumba kaunti hii ambayo ni kitovu cha uchumi wan chi.

Alichaguliwa na kuapishwa kama gavana wa nne wa Nairobi kupitia tikiti ya chama cha UDA baada ya kumshinda aliyekuwa mshindani wake wa karibu, Polycarp Igathe aliyekuwa akipimana nguvu naye kupitia chama tawala cha Jubilee.