"Niliumia sana, ilinitesa!" Jux afunguka kuhusu mahusiano yaliyomvunja moyo zaidi

Mwimbaji huyo alifichua kuwa mahusiano hayo yalitokea kabla yake kukutana na aliyekuwa mpenziwe Jacqueline Clifford.

Muhtasari

• Jux alikiri kuwa kusambaratika kwa mahusiano yake ya kwanza ni tukio ambalo liliwahi kumuumiza zaidi.

•Baadae Jux alijitosa kwenye mahusiano na malkia wa Bongo Vanessa Mdee kabla yao kutengana mwaka wa 2019.

Image: INSTAGRAM// JUMA JUX

Staa Bongo Juma Jux ameweka wazi kuwa kutengana kwake na Vanessa Mdee halikuwa jambo la kuvunja moyo zaidi katika maisha yake.

Katika mahojiano na Salama Na, Jux alikiri kuwa kusambaratika kwa mahusiano yake ya kwanza ni tukio ambalo liliwahi kumuumiza zaidi.

"Kuna mtu nilikuwa naye, ni maarufu pia sitaki kumtaja kwa sababu pia yeye ana maisha yake. Nilikuwa nimempenda sana, sana sio kidogo kutoka moyoni mwangu. Ni mapenzi yangu ya kwanza," alisema.

Msanii huyo wa RnB alisema mahusiano hayo yalitokea kabla yake kukutana na aliyekuwa mpenzi wake Jacqueline Clifford.

Alifichua kuwa mpenzi huyo wake wa kwanza alinyakuliwa na mwanaume mwingine wakati yeye alikuwa amesafiri. Alieleza kwamba mpenziwe huyo alitongozwa kwa pesa na gari na hatimaye akaamua kumtema.

"Alikuwa akinichezea akili yangu. Alipata mtu mwingine huku ambaye ana mahela yake akampa gari. Kumuuliza alikuwa akisema ni biashara zake zile. Ilifika hatua akaniambia kuna mtu yuko hivi na hivi, ananisaidia nyumbani kwetu, ananijengea na kujengea mamangu lakini simpendi," alisimulia.

Jux alidokeza kuwa mwanadada huyo hakutaka wasitishe mahusiano yao licha ya kuchumbiana na mwanaume mwingine.

Alikiri kuwa aliumia sana baada ya kutengana na mpenziwe huyo wa kwanza. Hata hivyo alichukua tukio hilo kama msukumo wa kufanya kazi kwa bidii zaidi.

"Ilinipa hasira, ikanipa nguvu ya kupambana nikasema suluhu sio kutafuta mwanamke mwingine ni kutafuta hela," Jux alisema.

Mwimbaji huyo alisema kuwa baada ya kugombana na mpenziwe huyo wa zamani walitengana na baadae akaanza kuchumbiana na Jackie.

"Mungu sio adhumani ikaenda enda ndio kipindi hicho ndio napata raha kidogo naoneka akatokea Jackie Cliff,"

Baadae Jux alijitosa kwenye mahusiano na malkia wa Bongo Vanessa Mdee kabla yao kutengana mwaka wa 2019.