Mtu asikuambie haiwezekani, Mungu pekee ndiye mwenye jibu la mwisho - Jalang'o

Asante Lang’ata nina deni milele!” Odiwuor alisema.

Muhtasari

• Jalang'o aliwausia wafuasi wake kwamba Mungu ndiye mpaji wa kila kitu na wasiache mtu yeyote kuwadunisha kwamba hawawezi.

Mbunge Phelix Odiwuor wa Lang'ata
Mbunge Phelix Odiwuor wa Lang'ata
Image: Instagram

Aliyekuwa mchekeshaji na mtangazaji Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o jana alikula kiapo bungeni kuwahudumia watu wa Lang’ata.

Baada ya kumaliza kula kiapo, mbunge huyo mpya alisema kwamba ushindi wake ni kwa watu wa Lang’ata pamoja na kuwezeshwa na Mungu.

Jalang’o alichukua fursa hiyo kusema kwamba uhsindi wake ni himizo kubwa kwa kila mtu mpambanaji wa chini huku nje ambaye amekuwa akiambiwa hawezi.

Aliwausia wafuasi wake na kila mtu ambaye anamtazamia kama himizo kuwa lolote linawezekana chini ya jua ukiwa na nia.

“Hii ni kwa ajili ya Mungu, kwa Lang’ata na kwa yeyote huko nje ambaye aliambiwa haiwezekani! Mungu pekee ndiye anayeweza kukufikisha hapa! Asante Lang’ata nina deni milele!” Odiwuor alisema.

Msanii huyo alijinyakulia ushindi kupitia chama cha ODM baada ya kumng’atua aliyekuwa mbunge Generali Nixon Korir wa UDA.

Baada ya kujishindia ubunge, Jalang'o alitangaza kuwaachia wafanyikazi wa chaneli yake ya YouTube hisa ili kujijenga kwa kile alisema kwamba bungeni atakuwa na majukumu mengi ambayo yatamzuia kujihushiza na chaneli hiyo.

Aliwataka kuchukua asilimia 80 ya mapato yote huku wakimpa asilimia 20.