Rais Ruto, tunangoja unga ya 70, WI-FI ya bure chini ya siku 100 - Jalang'o

Jalang'o alisema Ruto aliahidi hayo yote katika manifesto yake.

Muhtasari

• Sasa ni kufanya kazi na kuhakikisha kuwa rais kwanza ahakikisha yale yote ambayo alisema kwa manifesto yake lazima yatimie. - Jalang'o

Image: Instagram,Facebook

Mbunge mpya wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o amesema kwamba wao kama muungano wa upinzani rasmi wanasubiria kwa hamu na ghamu kuapishwa kwa rais William Ruto ili waanze kumhesabia siku za kwanza mia kuona kama atatimiza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni.

Ruto ambaye alipata umaarufu mkubwa kutokana na sera zake za kuwapa watu wa uchumi wa chini kipaumbele katika manifesto yake alisema katika siku za kwanza mia, mambo yote yatabadilika na maisha kurahisishika kwa faida ya watu hao wapambanaji.

Jalang’o akilizungumzia hili alisema kwamba hawatomwendea rahisi rais Ruto kwani watamshinikiza kutimiza ahadi hizo ili kuleta unafuu wa kimaisha katika watu wa chini kama alivyokuwa akiahidi wakati wa kampeni zake za Bottom Up.

Jalang’o alitetea uhusiano wake na Ruto na kusema kwamba walikuwa tu na tofauti za kisiasa ila sasa Ruto hatakuwa mtu wa kuegemea mrrngo fulani bali ni rais wa Wakenya wote na atahitajika kuleta unafuu si tu kwa makundi fulani bali kwa kila Mkenya mwenye maisha ya kupambana ‘hustler’

“Mahakama ya upeo ilisha toa uamuzi na maneno yao ndio mwisho. Sasa ni kufanya kazi na kuhakikisha kuwa rais kwanza ahakikisha yale yote ambayo alisema kwa manifesto yake lazima yatimie. Tunangoja sana unga ya shilingi 70, alisema na kutuahidi, tunangoja WIFI ya bure na vocha, tunangoja kila mtu atolewe CRB. Haya si maneno yangu bali ni ya rais William Ruto,” Jalang’o alisema.

Jalang’o alisema kwamba kwa sababu Ruto alitoa hizi ahadi zote, basi nao wataanza kumhesabia chini ya siku mia moja kuanzia Jumanne wiki kesho atakapoapishwa rasmi kama rais wa tano.

“Sasa ni yeye kutimiza tu, na hii ilikuwa chini ya siku 100 na baada ya hapo sasa kila kitu tutasubiri,” Jalang’o alitamka.