"Cool" Khalwale afurahishwa na unenguaji wa Azziad kwa kibao 'Vaida'

Vaida ni wimbo wa Kiluhya ambao umetungwa na Harry Richie na umetrend sana wiki hii

Muhtasari

• “Hapa umewakilisha jamii ya Waluhya ipasavyo,” Ondu Peter aliandika.

Seneta Khalwale afurahishwa na unenguaji wa Azziad
Seneta Khalwale afurahishwa na unenguaji wa Azziad
Image: Twitter

Katika wiki moja iliyopita, kumekuwa na klipu kadhaa haswa kwenye mtandao wa TikTok watu mbali mbali wakifanya maigizo ya wimbo mmoja wa Kiluhya ambao umetrend sana.

Wimbo huo kwa jina Vaida ulioimbwa na msanii chipukizi Harry Richie umewapata wengi walikatika nao na kupakia klipu zao kweney mitandao mbali mbali ya kijamii.

Mwanatiktoker Azziad Nasenya ni mmoja wa wale walioufanya wimbo huo na hata kupakia klipu yake akisakata kweli kweli kwa kuzungusha kiuno chake kwa nguvu mpya.

Azziad alipakia klipu yake kwenye mtandao wa twitter na kuwavutia watu wengi waliofurahikia jinsi alivyochangamkia wimbo huo huku akiimba mtu atadhani yeye ndiye mtunzi halisi.

“Uluhya ulioko ndani yangu haungepinga nisifanye hii,” Azziad aliandika kwenye Twitter.

Watu walisambaza video hiyo kwa kuretweet na mmoja wa umati mkubwa ulioshiriki kuisambaza alikuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye aliipakia na kuisindikiza kwa neno “cool” kwa maana kwamba ameipa dole iko sawa sawa.

Hatua ya Khalwale kuisambaza ilizua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki wake huku wengine wakimtania kwamba amemtolea macho mwanadada huyo mdogo na wengine wakimpongeza kwa kusema kwamba anashiriki katika kuikumbatia tamaduni ya Kiluhya.

“Mwaka ni 2040, mtoto wa Khalwale na Azziad anaibuka kidedea katika mtihani wa KCSE,” mmoja kwa jina Otieno Opondo alitania.

“Tulisema kitu lazima kimuue mwanaume daktari yuko tayari kuhatarisha yote,” mwingine alisema.

“Hapa umewakilisha jamii ya Waluhya ipasavyo,” Ondu Peter aliandika.

Mheshimiwa Khalwale amekuwa akigonga vichwa vya habari haswa baada ya wanamitandao kuibua mjadala kwamba kila mwaka matokeo ya kitaifa katika shule za upili na msingi yakitangazwa, lazima aonekane akimsherehekea mmoja wa watoto katika familia yake.