"Nimeiba bwana, si mabwana" - Karen Nyamu amzima mwanamke aliyemuita mwizi wa wanaume

Awali mke wa kwanza wa Samidoh alionekana kumrushia dongo Nyamu kwa kusema kwamba michepuko wanafaa kuheshimu ndoa za wenyewe.

Muhtasari

• Jibu la Nyamu lilizua utani mwingi kwenye mitandao ya kijamii, baadhi wakimsifia kwa kujibu sahihi huku wengine wakimzomea mwanadada huyo aliyemkaripia Nyamu.

Seneta mteule Karen Nyamu
Seneta mteule Karen Nyamu
Image: instagram

Seneta maalum Karen Nyamu kwa mara nyingine tena amejipata katika mjadala baina ya wanamitandao ya kijamii baada ya kuamua kuvunja ukimya wake dhidi ya mtumizi mmoja wa mitandao aliyemkaripia.

Nyamu kupitia Instagram yake alipakia picha akionekana kumshukuru Mungu kwa kumfanya kuteuliwa na chama cha UDA kama seneta mteule.

“Katika muda wote umekuwa ukitengneza njia pasipo na njia, ninakuita mtengeneza njia,” Nyamu aliandika.

Wakili huyo ambaye hakuonekana kuwa na neno na mtu alijipata ghafla ameguswa na mtumizi mmoja wa mtandao huyo aliyemuita mwizi wa wanaume wa watu.

“Hello mwizi wa mabwana za watu,” mtumizi wa Instagram kwa jina Mercy Ramsey alimchokoza.

Nyamu safari hii hakulifumbia macho suala hilo la kuhusishwa na kuiba wanaume wa watu kwani kulingana na jibu lake, alionekana kukerwa kuongezewa mambo mengine.

Aliamua kumjibu Ramsey kwa kumrekebisha na kumkumbusha kwamba yeye hajawahi iba mabwana bali ni bwana mmoja tu.

“Ni bwana, si mabwana. Rudia sasa vizuri,” Nyamu alijibu mipigo.

Kulingana na jibu alilolitoa, alijua fika kwamba anazungumziwa kuhusu suala la mwanamuziki na polisi Samidoh ambaye jina lake lilivutwa tena kwenye mjadala baada ya mkewe Edday kuachia maoni yake kwenye wazo la mwanamitandao mmoja aliyezungumzia michepuko kukoma kuiba wanaume wa watu.

Jibu la Nyamu lilizua utani mwingi kwenye mitandao ya kijamii, baadhi wakimsifia kwa kujibu sahihi huku wengine wakimzomea mwanadada huyo aliyemkaripia Nyamu.

“Sijakataa nimeiba lakini sasa mbona uongezee idadi ya vitu nimeiba?” mchekeshaji Sleepy David aliandika.