Nakusihi kata mizizi ya fitina, weka mzee begani - Baba Levo amwambia Ommy Dimpoz

Ommy Dimpoz alisema hana mapenzi na babake kabisa kutokana na mzee wake kumtelekeza kipindi yuko mtoto.

Muhtasari

• Ommy Dimpoz aliweka wazi kwamab hawezi kumtambua babake na kuwa na mapenzi naye kutokana na kwamba mzee alimtoroka akiwa mtoto.

• Baba Levo amemsihi kuzika ya zamani na kumkubali mzee wake kwani baba ni yule yule tu.

Baba Levo amshauri Ommy Dimpoz kumsamehe babake
Baba Levo amshauri Ommy Dimpoz kumsamehe babake
Image: Instagram

Baada ya mtangazaji Mwijaku kuibua mapya kuhusu mzee aliyesemekana kuwa babake Ommy Dimpoz na Dimpoz akaja akamkataa kwamab hamjui mzee huyo, Leo asubuhi msanii huyo amefanya video moja ya uchungu sana akizungumzia sababu zilizomfanay kumkana babake.

Mzee huyo alionekana maeneo ya Sumbawanga akifanya biashara ya kuendesha bajaj na wengi walizua gumzo mitandaoni ni kwa nini mzee wa watu anachakarika vile hali ya kuwa mtoto wake Ommy Dimpoz anakula bata akitamba kwenye miji ya watu huko ughaibuni mpaka kupiga picha na mastaa wa soka wakubwa.

Kwenye video ile iliyomgharimu Dimpoz dakika nane na ushee, alisimulia jinsi matukio yalivyojitokeza mpaka kumkana babake kabisa na kukiri kwamba hana mapenzi naye hata kidogo.

Ommy Dimpoz alielezea kwamab mzee babake alimtelekeza mamake na hata majukumu yote kuyakwepa. Mzee huyo hata mamake Dimpoz alipofariki kipindi akiwa mdogo, hakuweza kufika hata msibani na wala hakuwahi kufuatilia kujua maisha ya Dimpoz yangeendeleaje baada ya msiba wa mamake.

Dimpoz kwa uchungu mno alielezea kwamba mzee alienda akaanzisha familia nyingine na yeye alilelewa na nyanya yake mpaka nyota yake katika muziki ilipokuja kung’aa. Alisisitiza kwamba hawezi kumdhamini mzee huyo na katu hana mapenzi naye.

Sakata hilo limezua maneno mengi mitandaoni ambako baadhi wamempongeza kwa hatua hiyo ya kumtelekeza mzee kwani yeye ndiye alikuwa wa kwanza kumuonesha kwamba hana haja naye.

Lakini kwa upande wa pili pia, wapo wale wanaohisi kwamba Ommy anafaa kuyasahau yaliyopita na kumshika mkono mzee wake kwani mtoto akikunyea kiganja hufai kukikata bali unaosha tu na maisha yanazidi. Baba Levo ni mmoja wa wale wanaoegemea mrengo huu wa ushauri.

“Ndugu yangu @ommydimpoz pamoja na yote uliyoongea kwa uchungu sana…!! Nakusihi kata mzizi wa fitina kamata mzee wako muweke begani…!! Nunua ist mpe aendeshe uber atoke kwenye bajaji…!! Coz sababu za baba kutomuhudumia mtoto ni nyingi na zingine huwa zinasababishwa na mama zetu pia…!! Nashuri usiingilie magomvi yao play party yako kama mtoto …!!! Na mungu atakuzidishia…!!! Mama alikubeba miezi tisa tumboni..! Huwezi jua baba alikubeba miaka mingapi kwenye korodani,” Baba Levo alitoa ushauri.