Ommy Dimpoz amkana babake mzazi "Simjui"

Mzee huyo alionekana kweney video akipigiwa magoti na Mwijaku na katika mahojiano, Dimpoz akasema hamjui kabisa kama babake.

Muhtasari

• Vyanzo vya habari vinasema kwamba mzee huyo alikimbia majukumu enzi Ommy akiwa mdogo na kuenda kuoa mke mwingine kipindi mamake Ommy alipofariki

msanii Ommy Dimpoz amkana babake mzazi
msanii Ommy Dimpoz amkana babake mzazi
Image: Instagram

Wiki jana, mtangazaji mwenye utata Mwijaku alipakia video kwenye mitadano yake ya kijamii akionesha kuzungumza na mzee mmoja ambaye alisema ni babake msanii maarufu Ommy Dimpoz.

Mzee huyo ambaye alionekana kuishi maisha ya kawaida mno alijitambulisha kama baba wa kumzaa Ommy ila licha ya mwanawe kutusua kimaisha, hajaweza kumsaidia kabisa.

Mwijaku alifanya kitendo cha kumtafuta babake Ommy Dimpoz baada ya msanii huyo kutamba kwenye mitandao ya kijamii akila bata mnono kule Uingereza katika uwanja wa Old Trafford wa Manchester United huku akipiga picha na wachezaji maarufu na hata kupakiwa kwenye instastory ya timu hiyo.

Katika video hiyo, Mwijaku alionekana kuanguka chini na kumpigia magoti mzee huyo huku akimtaja kama babake Ommy, mzee anayejishughulisha na biashara ya bajaj ili kupata riziki.

Mwanamuziki Ommy Dimpoz katika mahojiano alipokuwa anahudhuria hafla ya Mziki Mnene ambapo msanii Marioo alikuwa anatumbuiza, aliulizwa kuhusu mzee huyo na akamkana kabisa kwamba si babake na wala hamjui wala kumtambua achia mbali kumfahamu.

“Mimi sijui Mwijaku kamtoa wapi mzee yule na mimi nitamuuliza Mwijaku umemtoa wapi huyu maana mimi simjui kweli,” Ommy Dimpoz alisema hadharani.

Itakumbukwa muda fulani nyuma msanii huyo katika mahojiano na mtangazaji Salama aliwahi kuulizwa kuhusu ukaribu wake na babake naye alikataa kabisa kwamba hakuna ukaribu hata kidogo.

Vyanzo vya habari vinasema kwamba mzee huyo alikimbia majukumu enzi Ommy akiwa mdogo na kuenda kuoa mke mwingine kipindi mamake Ommy alipofariki. Ommy amekuwa akilelewa na nyanya yake na wengi wanahisi mzee huyo anajaribu kujitambulisha kama babake baada ya mafanikio yake.

Ila pia katika video ile na mwijaku, alimtaja mzee huyo kama mtu ambaye ana pesa zake na hahitaji kumuomba mwanawe Dimpoz hata senti.