(+video) Usimjibu kila mtu mitandaoni - Haji Manara amshauri Ommy Dimpoz

Haji anashauri haya baada ya sakata la Ommy na babake mzazi likiendelea kutokota.

Muhtasari

• Ommy Dimpoz amejipata katika zogo kubwa mitandaoni baada ya sakata la kumtelekeza babake kuibuka.

Aliyekuwa msemaji wa timu za soka za Simba na Yanga nchini Tanzania Haji Manara amemshauri mwanamuziki Ommy Dimpoz kukoma kutojihusisha na kuwajibu kila mtu mitandaoni.

Haji Manara alikuwa akimuusia Ommy Dimpoz haya wakati alihudhuria sherehe za siku ya kuzaliwa kwake, saa chache tu baada ya Ommy kuenda mitandaoni na kuachia video moja akielezea Sakata linalozungumziwa sasa hivi mitandaoni kati yake na baba yake.

Awali kulikuwa kumeibuka maneno kuwa licha ya Ommy kuishi maisha ya kifahari, lakini babake mzazi alikuwa ni kabwela wa kutupwa ambaye kipato chake ni kutafuta riziki kwa kufanya kazi ya kuendesha bajaji Sumbawanga.

Wengi walionekana kumzomea Ommy jambo lililombidi kuibuka na kulainisha mambo jinsi matukio yalivyojiri mpaka yeye na babake kufikia hali hiyo ya kutoonana jicho kwa jicho.

Ommy alisema kwamba hawezi kuwa na mapenzi na babake kwa sababu mzee huyo alimtelekeza na kumtenga kipindi akiwa mtoto na mamake alipofariki ilibidi amelelewa kwa nyanya.

Watu walitoa maoni mbali mbali wengine wakimshauri Ommy kushikilia msimamo wake huo huo huku wengine wakimtaka kukata mizizi ya ugomvi kati yake na mzee babake na kujirudi kumkwamua mzee kutoka lindi la umaskini.

Manara kwa upande wake alimtaka Ommy kukaa kimya na kukoma kujibu kila mtu mitandaoni kwani kuna wengine wanataka kutamba tu kwa jina lake kisa kawajibu.

“Ndugu yangu, ninakuwaza tu kitu kimoja, achana na kujibu kila mtu mitandaoni. Kuna kiwango ukifika basi kuwa watu huku chini wanataka kupambana ili wakuangushe mradi wapande. Hao hupaswi kuwajibu. Si kila mtu unafaa kumjibu. Kuna watu mitandaoni hata watukane vipi, usijibu. Ukijibu tu unamfanya watu wamjue,” Haji Manara alimshauri.