"Naanza kuwa mkubwa!" Zari azidiwa na mahaba anayopewa na mpenziwe mdogo

Mwanasoshalaiti huyo amemsifu mpenzi wake kwa kumwekea mazingira mazuri ya ukuaji.

Muhtasari

•Zari amebainisha kuwa mpenziwe mpya amemletea amani ambayo imemwezesha kukua na kung'aa zaidi.

•Aidha aliwasuta watu wanaotakia mahusiano yao mabaya huku akidokeza kuwa juhudi zao zote zimefeli.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasosholaiti na mfanyibiashara maarufu Zari Hassan amemsifu mpenzi wake Shakib Lutaaya kwa kumwekea mazingira mazuri ya ukuaji.

Katika video aliyochapisha kwenye TikTok, alibainisha kuwa mpenziwe mpya amemletea amani ambayo imemwezesha kukua na kung'aa zaidi.

"Mimi naanza kuwa mkubwa. Naona shavu. Nimejipa amani sana. Bwana Lutaaya unanipa amani sana  kwa maana, watu, ngojeni niwaambie kuhusu amani ya  akili, hiyo nawaambia hata ufanye nini, unakua mkubwa zaidi hata usipokula," Zari alisema katika video hiyo ambayo alipakia hivi majuzi.

Mama huyo wa watoto watano alimtaka mpenzi wake kuendelea kumpatia mahaba anayompa huku akimbainishia kuwa yanafanya kazi.

Aidha aliwasuta watu wanaotakia mahusiano yao mabaya huku akidokeza kuwa juhudi zao zote zimefeli.

"Bwana Lutaaya chochote unachofanya, ongeza zaidi. Niongezee dozi nyingine, chochote unachofanya kwa sababu zinafanya kazi, zinafanya kazi. Hata hao wanaoroga wamekata tamaa, wanahitaji kurejeshewa pesa zao. Bado nina amani, nendeni mkaombe kurejeshewe pesa zenu," alisema.

Zari amekuwa akitetea mahusiano yake na Lutaaya hasa kwa kuwa amekosolewa sana kufuatia utofauti wao wa kiumri.

Wiki chache zilizopita alifichua kuwa amempiku mpenzi huyo wake  kwa takriban miaka kumi.

"Mpenzi wangu sio mdogo. Ana miaka 30 anaelekea 31 Desemba mwaka huu. Yeye sio mdogo, anakaa mdogo. Mimi natimiza miaka 42 mwaka huu na huwezi kujua," Alisema.

Katika chapisho lake la awali mzaliwa huyo wa Uganda alibainisha kuwa maisha yake hayafungwi na sheria zilizowekwa na jamii.

Zari alisema kwamba yuko na haki kamili ya kumchagua mwanaume ambaye angependa kuchumbiana naye.

"Ukiniambia nichumbie nani na nisichumbie nani, nawajua wa aina hizo. Lakini hapa ndipo ninapoamua kubaki. Ni nini kinachokufanya ufikiri kwamba watu wengine hawana hadhi?,"  alisema.

Zari amekuwa akikejeliwa na kukosolewa sana baada ya kufichua mpenzi wake wa sasa takriban miezi michache iliyopita.

Alionekana na mpenzi huyo wake kwa mara ya kwanza katika ziara ya kikazi nchini Kenya na Tanzania.

Akiwahutubia waandishi wa habari baada ya kutua Tanzania, Zari alimtambulisha mwanaume huyo, sio tu kama mpenzi wake, bali pia kama mume wake.

“Huyu ni mume wangu, ni mume wangu, kesi kwisha!” Zari alisema