Njugush achukizwa na hakikisho la spika Wetangula kwa Wabunge kupata nyongeza ya posho

Jana Wetangula aliwaambia wabunge wasiwe na wasi wasi kwani tayari mazungumzo na tume ya kuratibu mishahara yameanza.

Muhtasari

• Na mimi kama spika wako nitahakikisha tumeishauri vyema SRC kuwa sio watu wa kukatisha tamaa bali ni wawezeshaji wa Wabunge kufanya kazi zao - Wetangula.

Njugush achukizwa na kauli za spika Wetangula
Njugush achukizwa na kauli za spika Wetangula
Image: maktaba

Mchekeshaji Blessed Njugush ameonesha kutoridhishwa kwake na matamshi ya spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula aliyewaambia wabunge kwamba ni muda wa kujivinjari na marupurupu ya magari ya kifahari pamoja na mikopo mingine.

Njugushi alipakia kwenye Instagram yake habari hizo kwamba spika Wetanguls aliwapa hakikisha wabunge kwamba atawapigania ili kupata marupurupu na mikopo ya magari pamoja na kuwekewa mafuta, huku akiwahakikishia kwamba mazungumzo na tume ya kuratibu mishahara SRC tayari yameanza.

“Hakuna mtu aliye na akili timamu atakayeingilia posho za gari lako, ulipaji wa mafuta kutoka umbali unakokaa na rehani yako na kila kitu ambacho umekuwa nacho kwa sababu hiyo ni haki yako. Na mimi kama spika wako nitahakikisha tumeishauri vyema SRC kuwa sio watu wa kukatisha tamaa bali ni wawezeshaji wa Wabunge kufanya kazi zao. Tunawahakikishia kuwa hakuna kitakachobadilika na ikibadilika haitakuwa kubwa," spika Wetangula aliwaambia wabunge.

“SRC watakuwa wameelezewa kabisa nimemualika mwenyekiti atakuwa hapa ila atakuja baada ya kufanya mawasiliano niliyowaambia,” Wetangula aliongeza.

Hakikisho hili la spika kwa wabunge lilimchukiza Njugush ambaye aliwakumbusha mashabiki wake kwamba ni wazi sasa bungeni hakuna mirengo ya kupigania haki za mnyonge bali wapo wenyewe tena pamoja na wanyonge huku chini watazidi kujipambania kivyao.

“Labda ni wakati mzuri wa kukukumbusha, uko peke yako ... wako pamoja. Hidhuru nimetafakari tu,” Njugushi aliandika.