Zabron Singers waeleza vile walipata mwaliko kutumbuiza hafla ya rais Ruto kuapishwa

Walisema kwamba familia ya rais Ruto iliwaeleza kuwa imekuwa ikibarikiwa na nyimbo zao kwa muda mrefu.

Muhtasari

• Kikundi cha Zabron Singers kuenda kutumbuiza kwenye uapisho wa rais haikuwa kazi rahisi kama tunavyofikiria - Mwalimu Japhet, mkuu wa kundi hilo.

Kundi la Zabron Singers wakiwa na rais Ruto
Kundi la Zabron Singers wakiwa na rais Ruto
Image: William Ruto

Kundu la wanafamilia wainjilisti kutoka Tanzania, Zabron Singers baada ya kurejea nchini mwao kutoka kutumbuiza katika hafla ya kuapishwa kwa rais Ruto, waliita mkutano na wanahabari na kuzungumzia mengi jinsi walivyopata mwaliko rasmi kuwa miongoni mwa watumbuizaji.

Kundi hilo lilisema lilifarijika sana kuitwa kwa mwaliko rasmi na kitengo kilichosimamia burudani siku ya kuapishwa kwa rais Ruto mapema mwezi Septemba.

“Kikundi cha Zabron Singers kuenda kutumbuiza kwenye uapisho wa rais haikuwa kazi rahisi kama tunavyofikiria. Unajua Kwenda kusimama uko kwa mheshimiwa hicho hakikuwa kitu kidogo. Tumefikiria kutoa shukrani kwa sababu hili limekuwa jambo la heshima kwetu na kikweli ni jambo la kuwatia moyo wasanii wengine kwamba tukizidi kutia bidi kazi zetu zitafika mbali zaidi,” kiongozi wa kundi hilo alisema.

Japhet ambaye ndiye msimamizi wa kikundi hilo alifunguka kwamba hapo nyuma walikuwa wanawasiliana na familia ya rais Ruto na walipopewa mwaliko ule walijifunza mengi sana.

“Tulikuwa tukiongea mawili matatu na familia ya rais Ruto wakawa wakituelezea namna ambavyo wamekuwa wakibarikiwa na nyimbo zetu na kingine ambacho walizungumza kuhusu kikundi cha Zabron Singers ni kwamba wamekuwa wakisikiliza kazi zetu na hata kututajia baadhi ya nyimbo ambazo kiukweli zimekuwa zikifanya vizuri,” Japhet alisema.

Familia ya Waimbaji wa Zabron wamefanya kazi kama familia na walianza kuimba mwaka 2006 lakini walianza kurekodi rasmi mwaka 2012 huku albamu ya kwanza ikiitwa Tunawakumbuka.

Mwaka wa 2013 walifanya albamu ya pili iitwayo Mkono wa Bwana, wimbo katika albamu hiyo ndio ulikuwa mkubwa na uliwaletea mafanikio makubwa sana ambao mpaka sasa una utazamaji kwenye mtandao wa YouTube zaidi ya milioni 45 na ndio wimbo ambao kila mara wakiitwa kwenye hafla za kutumbuiza wanaambiwa waimbe.