Kajala afunguka sababu ya kushiriki video ya Harmonize, Nitaubeba

Kajala ndiye alikuwa mhusika mkuu katika wimbo mpya wa Nitaubeba wake Harmonize.

Muhtasari

• "Nakupenda sana mpenzi ❤️Wewe ni kitu bora zaidi ambacho nimewahi kuwa nacho,” Kajala

Kajala amesema ni kwa nini alikubali kushiriki kwenye video ya Harmonize
Kajala amesema ni kwa nini alikubali kushiriki kwenye video ya Harmonize
Image: Instagram

Moja kati ya vitu vinavyozungumziwa pakubwa katika mitandao ya kijamii ukanda wa Afrika Mashariki ni video mpya kutoka kwa msanii Harmonize kwa jina Nitaubeba.

Harmonize alifanya kweli kutoka kwa micharazo ya maneno, midundo na hata ujumbe wenyewe ni maalumu kwa mtu anayempenda mia kwa mia.

Isitoshe pia katika video ambayo aliiachia usiku wa Jumatano, mhusika mkuu ni yeye pamoja na mchumba wake Fridah Kajala Masanja, na aliweka wazi kwamba video hiyo pamoja na wimbo wote aliutunga mahususi kwa ajili yake, miezi kadhaa baada ya kumvisha pete ya uchumba.

Kajala mwenyewe pia naye ametilia neno lake katika video hiyo ambayo inazidi kuzungumziwa, haswa kipande ambacho kinawaonyesha kama wamefunga pingu za maisha katika ufukwe.

Kajala alisema alikubali kufanya video hiyo kama vixen kwa njia ya kipekee kwa vile mpenzi wake alimtungia maalum.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kajala Masanja alimsifia Harmonize kwa weledi wake uliokolea katika kutunga mashairi ya kutia tabasamu kwa maisha yao ya kimahaba na kusema staa huyo wa Konde Gang ndiye kitu cha kipekee amabcho kimewaho kutokea maishani mwake zaidi ya miongo mitatu na ushee iliyopita.

“Ilinibidi nifanye video hii kwa sababu mchumba wangu aliniimbia. Nakupenda sana mpenzi ❤️Wewe ni kitu bora zaidi ambacho nimewahi kuwa nacho,” Kajala aliandika kwenye Instagram.

Kajala walirudiana na Harmonize baada ya miezi kadhaa ya kukunjiana kwa kile kilitajwa kuwa ni Kajala kugundua Harmonize alikuwa na njama ya kujaribu kuweka kwenye ghala ngano na makapi yake.

Kwa sasa, yeye ni meneja wa kazi za muziki za Harmonize na kuachia ngoma yenye ladha ya aina yake kama hiyo kunaonesha kweli kuwekwa kwake kama meneja si lele mama.