Willy Paul asema madai ya uongo kutoka kwa Diana Marua yalimwathiri kifikira

Mwaka jana Diana Marua alifanya video akisema Willy Paul aliwahi fanya jaribio la kumbaka.

Muhtasari

• "Iliniharibia sana, unajua madai ya uongo mambo yanaweza kukufanya, kabla watu wakuje kujua ukweli unakuwa umepoteza mengi sana,” Willy Paul alisema.

Willy Paul azungumzia kupitia unyongovu
Willy Paul azungumzia kupitia unyongovu
Image: YouTube screengrab

Kwa mara ya kwanza msanii Willy Paul amezungumzia jinsi ufichuzi aliouita wa uongo kutoka kwa Diana Bahati ulivyochafulia jina na kumsababishia unyongovu.

Mwaka jana mwanablogu Diana Marua alifanya video akilia na kumtuhumu msanii Willy Paul kwamba alimbaka miaka fulani nyuma. Video hiyo ilisambaa pakubwa katika mitandao huku wengi wakiamini Pozze alifanya kitendo hicho cha ukatili, kwa jinsi Marua alikuwa anaelezea matukio huku akilia kwa hisia kali.

Willy Paul alijitokeza na kukana matukio hayo vikali kwa kusema kuwa Marua alikuwa anamsingizia kwa nia ya kumchafulia jina na taaluma yake ya kimziki.

Katika tukio hilo ililoonekana kama filamu, wengi walilifananisha na Sakata la msanii kutoka Marekani ambaye sasa amepatikana na hatia ya kuwadhulumu wanawake kimapenzi, R Kelly.

Baada ya kuona kwamba mambo yalikuwa yanamponyoka mikononi huku madili yakimtoka, Paul alilazimika kuelekea mahakamani ambapo Marua aliamrishwa kuifuta video ile kutoka YouTube yake.

Pozze, kama anavyojiita amesema Sakata hilo lilimsababishia mambo mengi hasi na karibu ajipate katika msongo wa mawazo ila Mungu aliingilia kati na kumuinua tena.

“Mchozi yangu hakuna mtu ameshawahi kuyaona kando na siku moja tu kwa kitu kilichoniumiza sana. Iliniharibia sana, unajua madai ya uongo mambo yanaweza kukufanya, kabla watu wakuje kujua ukweli unakuwa umepoteza mengi sana,” Willy Paul alisema.

Willy paula alisema kwamba madai hayo yalipompeleka chini, Mungu aliingilia kati na hapo ndio wimbo wake wa Toto ulikuja ukafanya vizuri sana na tangia hapo ngoma zingine pia zimekuwa zikipata mapokezi makubwa sana kutoka kwa mashabiki, kitu ambacho alisema ni Mungu tu alimpigania, kugeuza matatizo yake kuwa baraka.

Msanii huyo alifunguka kuwa kipindi hicho cha madai ya ubakaji kilikuwa kigumu na hata kwa afya yake ilikuwa katika hali ya hatari.

“Siwezi danganya, nilikuwa katika hali ya unyongovu kwa muda, hata sasa hivi bado kuna kitu kinazidi kuniumiza lakini ninaendelea kulifanyia kazi na kila kitu ni kazi ya Mungu,” Willy Paul alizungumza kwa hisia.