Eric Omondi aibuka na staili mpya ya nywele

Msanii huyo amekuwa akizama na kuibuka kwa mitikasi mipya kila wakati.

Muhtasari

• Omondi alisema kuwa huo ndio mtindo wake mpya wa nywele na kuwataka watu waweke maksi katika mtindo wake huo.

Omondi na staili mpya ya nywele
Omondi na staili mpya ya nywele
Image: Instagram

Kila mtu nchini Kenya atageuza shingo mara mbili mbili pindi tu jina Eric Omondi litakapotajwa, hii ni kutokana na umaarufu ambao mchekeshaji huyo amejilimbikizia ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki kwa takribani miongo miwili sasa.

Wengi wamekuwa wakisema wasanii haswa katika kitivo cha ucheshi nchini huja na kupotea kama umande, lakini kwa Omondi, yeye alitia guu katika Sanaa hii kudumu, wala hana mpango wowote wa kuonesha jukwaa la uchekeshaji mgongo.

Mchekshaji huyo amekuwa akitumia mbinu nyingi za kuhakikisha jina lake linazidi kukolea tena kwa herufi kubwa za dhahabu katika Sanaa ya ucheshi nchini.

Mitikasi yake imekuwa ikizungumziwa sana kutoka kuanza kuvalia nguo za kike na hata kujipodoa kama mtoto wa kike kwa jina Divalicious, mpaka kuigiza kama wanasiasa mbali mbali humu nchini akiwemo rais William Ruto na Raila Odinga.

Omondi kwa mara nyingine tena ameteka anga kwa njia tofauti baada ya kuzama na kuibuka na mtindo mpya kabisa wa nywele ambazo safari hii zinamtiririka kichwani kama manyoya ya farasi.

Omondi alisema kuwa huo ndio mtindo wake mpya wa nywele na kuwataka watu waweke maksi katika mtindo wake huo.

“Tazama,  Mtindo Mpya wa Nywele. NDIYO au HAPANA???” Omondi aliandika.