Willy Paul afurahia kufikisha wafuasi milioni moja YouTube

Pozee kama anavyojipamba mwenyewe alifika hatua hii kubwa muda mchache tu baada ya ngoma yake mpya na Jovial kutoweka YouTube.

Muhtasari

• Pozee sasa anakuwa msanii wa tatu katika safu ya kizazi kipya kufika hatua hiyo.

Image: Willy Paul

Msanii na mjasiriamali katika sekta ya muziki wa kizazi kipya nchini Kenya Willy Paul amekuwa wa hivi punde kufikisha wafuasi zaidi ya milioni moja nchini Kenya katika jukwaa la YouTube.

Pozee alifikisha wafuasi hao muda mchache tu baada ya Collabo yake mpya na msanii anayesemekana kuwa mpenzi wake pia Jovia kutoweka YouTube kwa njia zenye utata.

Ngoma hiyo ya Lalala ambayo ilikuwa mbichi kabisa ilitoweka kabla hata ya kumaliza saa 48 kwenye YouTube na mpaka habari hii ilipokuwa inaenda hewani bado hakuna upande wowote uliojitokeza kulizungumzia hilo. Haijulikani moja kwa moja kama ni wenye ngoma waliitoa au ni mtu alipeleka malalamishi ya hatimiliki kwenye wamiliki wa mtandao huo wakiteta kupelekea kufutwa kwake.

Mapema mwaka huu msanii Otile Brown aliweka rekodi kuwa msanii wa kizazi kipya kutoka nchini Kenya kuwahi kutokea kutia guu lake kwenye alama ya milioni moja ya ufuasi YouTube ambapo mtandao huo ulimpokeza baton ya dhahabu kama njia moja ya kusherehekea naye kwa hatua hiyo.

Miezi michache iliyopita pia msanii Bahati Kenya aligonga wafuasi milioni moja kwenye YouTube na Pozee amejinafasi katika tatu bora ya orodha ya wasanii wa kizazi kipya nchini Kenya kuwa na ufuasi wa watu zaidi ya milioni.

Itakumbukwa Paul na Bahati wamekuwa ni washindani wa tangu enzi za nyuma kabisa wakianza usanii ambapo wote walianza kama wasanii wa injili kabla ya kugura na kufuata kile wengi walikilinganisha na maji safi kwenye sanaa ya miziki ya kidunia.

Paul mwaka wa 2013 collabo yake na msanii Gloria Muliro ilishinda tuzo Groove Awards ambapo pia miaka michache mbele Bahati alitamba kwa kutuzwa msanii bora wa kiume katika tuzo hizo ambazo zilikuwa zinafanyika kila mwaka kuwatambua wasanii wa injili na michango yao katika kueneza neno la Mungu.