Mwambie Ruger asitishe hafla yake - Eric Omondi amwomba Tems

Alhamisi Tems aliandika kwa mshangao mkubwa kuwa hangeweza kuja Kenya kutumbuiza kwenye hafla iliyopangiwa Octoba 15.

Muhtasari

• Mcheshi huyo alimuomba Tems na wanamuziki wa mataifa mengine kutulia nchini mwao ili wanamuziki wa Kenya waweze kujikusanya na kujiinua katika sekta ya muziki.

• Omondi aliwaonya mapromota kuwa hatapumzika na atahakikisha kuwa hafla zozote watakazopanga hazitafaulu hadi watakapoamua kuwaweka wasanii wa Kenya kwanza.

Tems Baby// Eric Omondi

Mchekeshaji wa Churchill Eric Omondi afurahia tukio la mwanamuziki wa Nigeria, Tems kusitisha hafla yake ya Tukutane Festival iliyokuwa ifanyike nchini Kenya Octoba 15.

Omondi alimshukuru Tems kwa kuangazia suala la wanamuziki wa mataifa mengine kupata mamlaka ya kuandaa hafla wanavyotaka huku Kenya, jambo ambalo Omondi amekuwa akilipinga vikali.

Mcheshi huyo alimuomba Tems na wanamuziki wa mataifa mengine kutulia nchini mwao ili wanamuziki wa Kenya waweze kujikusanya na kujiinua katika sekta ya muziki.

"Waambie mandugu zako wasije Kenya kwa sasa ili msitukanyage wakati huu ambao hatuko sawa. Mtulie kwanza ili tuweze kupona na kujirudisha," Omondi alisema.

Kama tu alivyokuwa akifoka hapo awali kuhusu hafla ya Ruger, Omondi alisisitiza kuwa Ruger pia hafai kungojea kuhudhuria hafla yake.

"Tuonyesha mema na undugu kwa kumwambia Ruger asitishe hafla yake na arudi nchini Nigeria. Mungu akubariki," Omondi alimsihi Tems.

Aliwaomba wasanii wakubwa wa nchi zingine pia kutoandaa hafla nchini Kenya mpaka wakati ambao Kenya itakuwa sawa kwenye sekta yake ya muziki.

Omondi pia aliwapa wanamuziki hawa muda wa mwaka mmoja wa kutotembelea Kenya ili tuweze kufikia nchi nyingine kimuziki.

Wasanii aliwataja kuwa wasiofaa kufanya ziara ya kimuziki nchini ni pamoja na  Davido, Konshens, Wizkid, Diamond Platnumz, Tiwa Savage, Burna Boy na Tems.

Aliwaambia kuwa wanaweza kutembelea Kenya baada ya mwaka huo mmoja aliowapa ndipo tutakuwa kwenye lengo moja nao.

"Mandugu zangu, tunawapenda na kuwathamini lakini mtupe wakati mdogo ili turekebishe mambo kwenye nyumba yetu. Hatuko sawa," mchekehaji huyo anayejitambulisha kama rais wa ucheshi Afrika aliwasihi.

Aliwaambia waandaaji wa hafla za Kenya na mapromota kuwaunga mkono wanamuziki wa Kenya kabla ya kuwaunga mkono wasanii wa nchi zingine.

Omondi alisema mapromota wa Kenya ndio wanaosababisha shida zilizomo nchini na katika sekta ya muziki wa Kenya.

Mcheshi huyo aliwaonya mapromota kuwa hatapumzika na atahakikisha kuwa hafla zozote watakazopanga hazitafaulu hadi watakapoamua kuwaweka wasanii wa Kenya kwanza.

"Ni jambo la kutumia akili ya kawaida tu. Wapatieni nafasi na kuwaunga mkono watoto wa kutoka kwenye nchi tuliyozaliwa . Msikuwe wapumbavu," alisema.

Omondi alisema kuwa mapromota hao kuwalipia wasanii wa nchi zingine ndege, mahali pa kukaa na kuwakaribisha humu nchini licha ya kuwalipa wasanii wa Kenya vijishilingi ni jambo ambalo hatatulia likiendelea.

Aliwaambia wanamuziki na mapromota kuwa anawapa mwaka mmoja wa kujipanga ili waweze kujijenga na kuujenga muziki wao.

"Lazima tufufue, tujipe jina mpya na kufanya mambo mapya! Wapeni wanamuziki wa Kenya heshima, msiwadharau ni kama wao ni wanamuziki ambao hawajafaulu. Mnakuwa wenye roho chafu, msinijaribu mimi," mcheshi huyo alifoka.