Vera Sidika afichua kiasi cha pesa alichotumia kufanyiwa upasuaji wa matiti

Mwanasoshalaiti huyo aliweka wazi kuwa aliweza kumnyonyesha bintiye bila matatizo yoyote.

Muhtasari

•Vera alisema kuwa alitumia zaidi ya shilingi milioni mbili kufanyiwa upasuaji huo ambao ulifanyiwa nje ya nchi ya Kenya.

•Pia aliweka wazi kuwa aliweza kumnyonyesha bintiye bila matatizo yoyote kwani alichagua upasuaji ambao ungemwezesha kunyonyesha bila tashwishi yoyote.

Vera Sidika

Mwanasosholaiti Vera Sidika amefichua kiasi cha pesa alizotumia kufanyiwa upasuaji wa kuongeza matiti yake.

Akijibu maswali kwenye ukurasa wake wa Instagram, mke huyo wa Brown Mauzo alisema kuwa alitumia zaidi ya shilingi milioni mbili kufanyiwa upasuaji huo ambao ulifanyiwa nje ya nchi ya Kenya.

"Ilinigharimu dola elfu 20,"alisema

Mama huyo wa mtoto mmoja alikiri kuwa matiti yake sio asili kikamilifu na kueleza alifanyiwa upasuaji ili kuyaongeza ukubwa.Pia alifichua kuwa alifanyiwa upasuaji mwingine wa kurekebisha meno yake.

Pia aliweka wazi kuwa baada ya kujifungua bintiye mwaka jana, aliweza kumnyonyesha bila matatizo yoyote kwani alichagua upasuaji ambao ungemwezesha kunyonyesha bila tashwishi yoyote.

Sidika alipoulizwa kama matiti yake bado yako imara hata baada ya kujifungua alisema kuwa  hayajawahi kulegea licha ya kumnyoyesha mtoto wake.

Wiki iliyopita, Sidika alikuwa ametangaza kuwa alifanyiwa upasuaji wa kuyapunguza makalio yake, jambo liloibua gumzo kubwa miongoni mwa wanamitandao. Baadae hata hivyo ilifichuka kuwa alikuwa akitafuta kiki kwa minajili ya wimbo wake mpya.

"Huku mitaani kulikuwa kumeanza kuchosha , wakenya walikuwa hawana jambo la kuongelea kwa wiki. Ilikuwa inaburudisha sana," Sidika alisema akieleza ni kwa nini aliwatania Wakenya kuwa amebadilisha umbo lake.

Mwanasosholaiti huyo alifichua kuwa makalio yake makubwa ni ya asili na kuweka wazi kuwa hakufanyiwa upasuaji wowote.

Sidika pia aliongeza kwamba alikuwa akiona haya kwa kuwa na makalio makuwa kabla ya kuwa maarufu na hilo lilibadilika baada ya yeye kuhamia jijini Nairobi na watu kumsifia akaanza kujivunia.

Mke huyo wa Brown Mauzo alijizolea umaarufu baada ya kushirikishwa kwenye video ya wimbo wa You Guy wa P-Unit na Collo.

Sidika alisema kuwa baada ya wimbo huo kuvuma ndipo alipojulikana na watu wa tabaka mbalimbali.