"Tulieni tu mtaona, wekendi bando za kutosha" - Vishy adokeza kurudiana na Stevo Simple Boy

Pia alisema kwamba hakuna mtu ambaye anaweza ziba pengo lake katika maisha ya Stevo Simple Boy.

Muhtasari

 
• “Ninyi tulieni tu, ngoja mtaona maneno, wekeni bando la kutosha kwenye simu zenu msiwe na wasiwasi,” Vishy alisema.

Vishy adokeza kurudiana na Stevo Simple Boy
Vishy adokeza kurudiana na Stevo Simple Boy
Image: Instagram

Mwanablogu wa YouTube na ambaye pia mwanafasheni Prity Vishy ametupa bomu la moto kwenye himaya ya aliyekuwa mpenzi wake wa muda mrefu msanii Stevo Simple Boy.

Katika mahojiano ya kipekee na kituo kimoja cha redio humu nchini, Prity Vishy alipigigwa simu na kucheka kwa furaha baada ya kupasuliwa taarifa kwamba Stevo Simple Boy na mpenzi wake mpya Gee wametengana.

Ikumbukwe wikendi iliyopita, Gee ambaye alikuwa ‘mpenzi’ wa Stevo Simple Boy na hata kuchagiza kwamba wangefunga ndoa alifunguka wazi na kusema kuwa hakuna na mapenzi na msanii huyo bali uwepo wao pamoja ilikuwa ni tu kiki pamoja pia na mitikasi ya kibiashara kwa ajili ya kusukuma ngoma yake mpya ya Wedding Day.

Alifunguka kwamba mkataba wao ambao ulikuwa ni wa kibiashara lakini uliokuwa unaigizwa kana kwamba wao ni wapenzi wa chanda na pete ulikamilika wiki jana na kuwa hakuwahi kuwa na hisia na msanii huyo wala hawakuwa na mkataba wa kimapenzi.

Pritty Vishy akizungumzia sakata hilo jipya, alitamba na kujipiga kifua kwamba yeye tangu awali alikuwa anajua Simple Boy na Gee hawangeenda mbali, iwe walikuwa pamoja kimapenzi au kibiashara alikuwa na uhakika mia kwa mia kwamba hawangedumu.

Vishy kwa mikogo ya tausi alisema kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kumfanyia Stevo Simpole Boy kile ambacho yeye alikuwa anamfanyia na kusema kwamba daima pengo lake katika maisha ya Simple Boy litabaki kuwa wazi kwani hapajatokea mtu na hapatawahi tokea mtu wa kuliziba pengo lile.

“Mimi nafasi yangu haiwezi kuzibwa kabisa, hakuna mtu anayeweza kufanya kile ambacho nilikuwa nafanya kwa Stevo Simple Boy,” Pritty Vishy alisema kwa madaha.

Aidha alipoulizwa kama huenda hivi karibuni jamii ya wanamitandao ya kijamii watawaona pamoja, Pritty Vishy alidokeza kuwa huenda hivi karibuni wakawa pamoja tena kwa kuwatania watu kwamba wawe wapole na kusubiri.

“Ninyi tulieni tu, ngoja mtaona maneno, wekeni bando la kutosha kwenye simu zenu msiwe na wasiwasi,” Vishy alisema.