Abdukiba amkubali Harmonize, aimba wimbo wake 'Amelowa' kwao jukwaani

Naeza nikasema kwamba ninakubali kazi zake ambazo anafanya, zinaonekana, anajituma - Abdukiba.

Muhtasari

• Wimbo ambao nimeuimba pale juu (Amelowa) ni wimbo ambao umeniteka, kuna vitu ambavyo vinajirudia kwenye kichwa - Abdukiba.

Abdukiba akitabasamiana na Harmonize
Abdukiba akitabasamiana na Harmonize
Image: Instagram

Msanii Abdukiba amemlimbikizia sifa na kumvisha koja la maua msanii Harmonize baada ya kutumbuiza kwenye shoo huko Mtwara.

Ifahamike kwamba Mtwara ndio nyumbani kwao Harmonize na Abdukiba ambaye ni kakake Alikiba kutoka lebo pinzani ya Kings Music alikuwa na shoo moja matata katika mji huo.

Alifurahi mapokezi ya mashabiki ambao walimkaribisha jukwaani kwa mbwembwe na kuimba pamoja naye nyimbo zake alipokuwa anatumbuiza.

Kikubwa kilichowateka watu ni pale alipoamua kuimba wimbo wa Harmonize ‘Amelowa’ jukwaani na umati wa watu ukasisimika ajabu, asikwambie mtu!

Baadae alipomaliza kutumbuiza alifanya mahojiano na wanablogu na kuzungumzia kitendo chake cha kuimba wimbo wa Harmonize, ambapo aliweka wazi kwamba anamkubali sana msanii huyo bosi wa Konde Music na kukiri kuwa Harmonize ana kipaji kikubwa sana kinacholenga kuipeleka nchi mbali kimuziki.

“Harmonize ni mtu ambaye wakati mwingi ninasikiliza nyimbo zake, hususan wimbo ambao nimeuimba pale juu (Amelowa) ni wimbo ambao umeniteka, kuna vitu ambavyo vinajirudia kwenye kichwa. Halafu pia niko kwao na sikuona vibaya kuonesha upendo kwamba ingawa hayuko bado tunaweza kuonesha heshima kwa mfalme wao,” Abdukiba aliweka wazi.

“Naeza nikasema kwamba ninakubali kazi zake ambazo anafanya, zinaonekana, anajituma na kupambana na pia anaonesha anataka kuipeleka nchi sehemu gani,” aliongezea msanii huyo kakake na Alikiba.

Alisema kwamba kando na yeye kutaka kujua kuwa Harmonize anakubalika kwao kwa kuimba wimbo wake, pia alifanya vile kwa sababu anajua fika Harmonize ana kipaji kikubwa sana.