Uchambuzi wa 'Nawaza' ya Diamond na 'My Way' ya Harmonize - Ubora katika utunzi wa nyimbo!

Wasanii hao wawili wlaidhihirisha ubora wao katika kuwateka mashabiki kupitia utunzi bora wa mashairi ya muziki.

Muhtasari

• Diamond kupitia wimbo wake wa Nawaza, alitikisa tasnia baada ya kuelezea mambo mengi kwa njia ya kuimba na kuwafurahisha wengi.

• Vile vile, Harmonize naye wiki iliyopita alikuja na dude moja kali ambalo limesisimua wengi kwa njia alivyohadithia matukio katika maisha yake.

Harmonzie, Diamond Platnumz
Harmonzie, Diamond Platnumz
Image: Instagram

Muziki wa wasanii kutoka Tanzania unazidi kupenyeza mpaka vijijini nchini Kenya, si kwa sababu Kenya hawana wasanii wa kuwateka mashabiki wao, bali kwa asilimia kubwa ni kutokana na weledi mkubwa katika kujieleza ndicho kinachofanya muziki wa Bongo kupendwa Kenya.

Wasanii Diamond na Harmonize kwa siku za hivi karibuni wameonesha jinsi walivyokubuhu katika kuandika mashairi ya kujieleza kimaisha, nyimbo am bazo zimeibuka kuwa pendwa zaidi katika mkusanyiko wa ngoma zote ambazo wamezitoa kwenye albamu.

Itakumbukwa miezi kadhaa iliyopita, msanii Diamond aliachia albamu fupi yake kwa jina FOA na katika nyimbo nyingi zilizokuwepo, ngoma moja kwa jina ‘Nawaza’ ilizungumziwa sana huku wengi wakiifurahia.

Katika Nawaza, Diamond alitumia vina vya tafsiri kuelezea uhusiano wake haswa na wasanii wenzake kimuziki ambapo katika vesi moja alisikika akisema kiini cha yeye kutotulia katika ndoa, pia alizungumzia sababu ya bifu yake na Alikiba na pia kumkandia harmonize kwa kuanzisha uadui naye.

“Nimejifunza binadamu kweli hawana jema, yaani mtoto unaemtunza ndio anakuombea ukilema…Niliowaza leo nilishawaza sana mimi na Kiba ugomvi kipi, nikagundua ni ushamba na ujana wa kugombania mashabiki……Nilichoshindwa kuoa kipi, nikagundua naepusha lawama maana najijua kwa kucheat,” ni baadhi ya maneno kwenye ngoma ya Nawaza ya Diamond ambayo kwa kweli msanii huyo alijieleza makubwa ambayo yalionekana kujibu baadhi ya maswali mengi kwenye vichwa vya mashabiki wake.

Kwa upande wake, Harmonize mwishoni mwa wiki jana aliachia albamu yake ya tatu katika taaluma yake ya muziki na wimbo mmoja pia uliibuka kuwa pendwa zaidi na mashabiki wake.

Wimbo huo kwa jina ‘My Way’ msanii Harmonize anajieleza jinsi anavyotaka watu wampe nafasi ya kuendesha maisha yake kwa njia anayoitaka mwenyewe na pia kujieleza kwa njia ile ile ya Diamond – akilenga kujibu baadhi ya maswali ambayo yanawaatuza mashabiki wake na ambayo hajawahi kuyabibu bayana.

Alianza kwa kuzungumzia jinsi mapenzi yake yalivyong’oa nanga na mwigizaji Jacqueline Wolper na mpaka alivyokuja kukutana na Kajala ambaye kwa sasa ni meneja wake.

Kuachana kwake na Wolper kulingana naye ni kuogopa kubishana na wanaume wengine na ndio maana akaamua kumpa moyo wake Muitaliano Sarah ambaye pia walitengana baada ya muda mrefu.

“Nikampa Sarah roho kulipiza kisasi, labda niseme ni mambo ya ujana ama pengine nyota zilipishana, kila siku tukawa tunagombana,” Harmonize aliimba.

Pia alizungumza kilichootesha uadui baina yake na Rayvanny katika moja ya mstari ambapo anamuita kama Dogo wa Mbeya aliyesambaza picha za uchi wake na binti Paula.

Kama hiyo haitoshi, msanii huyo pia anazidi kutema bomu kwa Diamond huku akisema kwamba kwa sasa yeye watu anaowajali ni watu wake wa karibu na kusema kwamba hata hakuwa na wazo la kuwa na ugomvi naye bali ni yeye aliingiwa na kiwewe kuogopa Harmonize kumzidi kimuziki.

“Ninachojali watu wangu wa karibu, hata huyo ndugu yenu sikutaka vita naye, ni presha kuhofia nampita,” aliimba.

Ama kwa kweli wasanii wa Bongo wamebobea katika utunzi wa mistari yenye vina vya kishairi vinavyorahisisha kujieleza kwao kwa njia ya kuvutia mno.