Umetangaza ujauzito wa 2, Jux ataandika wimbo wa kulia" mashabiki kwa Vanessa Mdee

Vanessa alipotangaza ujauzito wake wa kwanza, Jux aliandika wimbo wa hisia kwa jina Sina Neno kumtakia mema.

Muhtasari

• Mapema wiki hii Vanessa Mdee alitangaza ujauzito wake wa pili na mwanamuziki Rotimi kutoka Marekani.

Vanessa na mpenzi wake wa zamani JUma Jux
Vanessa na mpenzi wake wa zamani JUma Jux
Image: Instagram

Kama wewe ni mfuatiliaji wa karibu wa Sanaa ya muziki wa Bongo Fleva kutoka Tanzania, basi utakuwa na ufahamu kubwa kwa muda mrefu wasanii Juma Jux na Vanessa Mdee walikuwa wapenzi wasioweza kutenganishwa hata kwa dakika moja.

Ila mapenzi yao yalikuja kukamilika kwa njia isiyotarajiwa na wengi ambapo Vanessa Mdee alihamia nchini Marekani na kuolewa na msanii Rotimi.

Japokuwa Jux na Mdee walikuwa pamoja kwa muda mrefu, hawakuweza kupata mtoto ila miezi kadhaa tu baada ya kuweka wazi uhusiano wake na Rotimi, Vanessa Mdee alitangaza kubeba ujauzito wa mwanawe wa kwanza na Mmarekani mweusi huyo mwenye asili ya Nigeria.

Hili lilizua mjadala mkali baadhi wakimshtumu Jux kuwa huenda alifeli kumzalisha Mdee na ndio chanzo cha kumtoroka na kuenda Ulaya kuolewa huko.

Baada ya Rotimi na Mdee kutangaza ujauzito wa mwanao wa kwanza, msanii Juma Jux aliingia studioni na kuandika wimbo mmoja wenye hisia kali za kuelezea jinsi alivyopokea taarifa hizo na hata kujikosha kwa kusema kwamba anawatakia kila la kheri katika uzazi wao. Wimbo huo ulikwenda kwa jina ‘Sina Neno’

Haya, mapema wiki hii, wapenzi hao walioko Marekani walitangaza tena ujauzito wao wa pili, takribani miaka miwili tu baada ya kupata mtoto wa kwanza.

Taarifa hizo jap zilitangaziwa nchini Marekani lakini Afrika Mashariki walizichukua kama zao na kuanza kumchamba Jux, wengine wakizua utani kwamba huenda ataandika wimbo mwingine tena wa kuzungumzia ujauzito wa pili wa Vanessa Mdee, kama alivyofanya katika wimbo wa Sina Neno.

Mdee kupitia Instagram yake alipasua mbarika kuwa anatarajia mtoto namba 2 ila Wabongo wakaanza kumueleza kinagaubaga jinsi Jux atapokea ujumbe huo.

“Ni muda sasa kwa Jux kuingia studio ili kuachia EP ya pili baada ya Sina Neno,” Isan Superboy alitania.

“Jux sio muda mrefu atatoa nyimbo tena,” mwingine alisema.

“Jux ameshaanza kuandika vesi huko,” Ms Diva alisema.