Vivianne adokeza Sam West anataka kurudiana naye, aomba ushauri

Msanii huyo alidokeza kwamba mpenzi waliyeachana miaka miwili sasa anataka kumrudia na kuomba ushauri kutoka kwa mashabiki wake.

Muhtasari

• Baadhi walimshauri kutokubali kurudiana naye kabisa kwani hatua hiyo itakuwa kama ya kumrudisha nyumba kimaendeleo.

Vivianne na muonekano mpya baada ya kuvunjika kwa ndoa yake
Vivianne na muonekano mpya baada ya kuvunjika kwa ndoa yake
Image: Instagram

Mwanamuziki wa Kenya, Vivianne ameachia ujumbe changamano kupitia ukurasa wake wa facebook – ujumbe ambao unadokeza kuwa huenda mchumba wake wa muda mrefu Sam West anataka warudiane.

Dokezo hilo linakuja wiki chache baada ya kuthibitisha kutengana kwao kufuatia miezi kadhaa ya uvumi kutoka kwa mashabiki wa kazi zake za kimuziki.

Vivianne ambaye alinyoa baada ya mzigo wa kuvunjwa moyo kuonekana kumlemea kichwani amekuwa kwa siku kadhaa akidokeza kwamba huenda anapitia tatizo la msongo wa mawazo kufuatia kuvunjika kwa uhusiano wake na Sam West.

Aliuliza mashabiki wake kutoa ushauri wa kile watakachokifanya kama wapenzi wao wa zamani wanataka kurudiana nao – katika kile kilionekana kama swali la kuwataka watu kujivika katika viatu vyake kwa hali anayoipitia sasa.

"Ni nini kingekufanya umrudishe mpenzi wa zamani ambaye alikuwa hayupo na sasa anataka kurudi baada ya mwaka mmoja au miwili ya kuwa mbali na wewe," aliweka kwenye mitandao yake ya kijamii.

Wafuasi wake walitoa maoni tofauti katika majibu yao.

“Anarudi kifedha ama kimapenzi. Kumrudia Ex wako ni kama kufanya harakati ya kujitia kitanzi, huwa haiishi vyema,” Maggie Mwajuma alimwambia.

“Mambo Na ex wachana..hautakua ukiendelea kung'ang'ania yaliyopita..acha yaliyopita yawe yamepita na ushughulikie sasa na yajayo..” Douglas Babu alimshauri.

“Kiburi cha watu wengi ndiyo hutuma waishi kujuta,,,mapenzi hayana mwisho,,,ni ile tu watu wanakataa,,,,kama unampenda mtu,,,usikatae,” mwingine alikuwa na mawazo tofauti.

Mnamo Oktoba 2022, Vivian alisema kuondoka kwa mume wake kumemsababishia maumivu licha ya juhudi za kujikaza kufanya kama mambo yako sawa.

“Siko vizuri, nimekuwa nikipata msaada lakini wakati mwingine naanguka. Moyo wangu ni mzito sana. Mtu alituacha na sasa anatuchukia. Nimekuwa nikijaribu kujenga upya lakini nimekuwa nikijiuliza kwanini. Tafadhali niombee kwa sababu mimi bado ni mama,” Vivian alisema.

 

Sam West alimchumbia Vivian wakati wa hafla ya moja kwa moja ya runinga, na wawili hao walikuwa wamechumbiana kwa miaka. Walikuwa na familia iliyochanganyika, ambayo watu wengi waliipenda. Wakati Vivian alikuwa na binti, Sam West alikuwa na mtoto wa kiume kutoka kwa uhusiano wa awali.