Rais mstaafu ahudhuria uzinduzi wa albamu ya Ommy Dimpoz

Ommy alisema kuwa alimwalika rais huyo mstaafu kutokana na mapenzi yake katika kazi za Bongo Fleva.

Muhtasari

• Lakini pia amekuwa mshauri na baba kwangu kwani hata wakati nilipokuwa naumwa alikuwa akiwasiliana nami mara kwa mara - Dimpoz alieleza sababu ya kumualika rais mstaafu.

Ommy Dimpoz
Ommy Dimpoz
Image: Ommy Dimpoz

Msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz Jumamosi Novemba 5 alizindua albamu yake mpya jijini Dar es Salaam.

Ommy ambaye amekuwa mbali kidogo na muziki kwa muda mrefu kutokana na shughuli mbalimbali haswa lile tukio la ugonjwa lililomwea mkekani kwa miezi kadhaa alirejea kwa kishindo ambapo albamu yake ilizinduliwa katika sehemu tofauti jijini.

Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, msanii huyo ambaye pia ni miongoni mwa majaji sifika sana katika mashindano ya BSS alisema kwamba alimwalika rais mstaafu Jakaya Kikwete kama mgeni wa heshimu kuzindua albamu hiyo.

Albamu hiyo aliyoipa jina la Dedication, itakuwa ni albamu yake ya kwanza kutoa tangu alipoanza muziki miaka kumi iliyopita.

Akieleza sababu za kumualika Kikwete, Ommy alisema ni kutokana na kuwa mmoja wa viongozi anayependa muziki wa Bongo Fleva na kwamba amekuwa karibu naye kama baba yake.

"Mzee wetu huyu amekuwa akipenda sana kazi tunazozifanya, hivyo nikaona nimualike kuja kushuhudia albamu yangu hiyo ya kwanza na kupata maoni yake. Lakini pia amekuwa mshauri na baba kwangu kwani hata wakati nilipokuwa naumwa alikuwa akiwasiliana nami mara kwa mara na kunipa msaada wa hali na mali," alisema msanii huyo.

Albamu ya Dedication ina jumla ya nyimbo 15 ambapo tayari ameshatoa ngoma ya kusafisha njia kwa ajili ya albamu yenyewe kwa jina  Vacation aliyosema video yake ilifanyiwa Uhispania.

Alisema kwamba hakutaka kuachia ngoma moja baada ya nyingine na ndio maana akaamua kuziweka zote kwenye albamu kutokana na matakwa ya soko la muziki wa kizazi hiki.

"Tunakutana na wafanyabiashara mbalimbali huko duniani na unapotaka kufanya nao kazi wanakuuliza albamu yako ipo wapi, hivyo nimeona ni wakati sasa nami kutoa albamu ili nifanye biashara."

Sababu nyingine alisema ni kutokana na kuwepo kwa majukwaa mbalimbali kwa sasa ya kuuza kazi za muziki tofauti na huko nyuma ambapo walikuwa wakitegemea watu wawili watatu nchini kuwasambazia kazi zao.

Ommy kwa mara ya kwanza kwenye muziki alitambulika na wimbo wake wa Nainai na baadaye kuepua vibao vingine ikiwemo Baadaye, Me and You aliyoimba na Vanessa Mdee, Tupogo, Kajiandae na sasa akiwa anatesa na kibao cha Vacation, ambacho video yake ilitoka mwezi mmoja uliopita.