Ndege ya Precision yatolewa Ziwani Victoria baada ya takriban siku tatu

Ndege ya Precision Air ilipata ajali tarehe 6 mwezi wa Novemba kwa kutua Ziwani Victoria

Muhtasari

• Mabaki ya ndege hiyo yaliondolewa majini siku ya Jumanne huku wataalamu wa safari za ndege wakiendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo. 

• Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 19 na wengine 26 kuokolewa kutoka majini katika zoezi lililoendeshwa na wavuvi wakishirikiana na maafisa polisi.

Precision Air

Ndege ya shirika la Precision Air iliyohusika katika ajali baada ya kuanguka  katika ziwa Victoria eneo la Bukoba,mkoani Kagera nchini Tanzania imeondolea majini. 

Mabaki ya ndege hiyo yaliondolewa majini siku ya Jumanne huku wataalamu wa safari za ndege wakiendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo. 

Mamlaka ya anga nchini Tanzania imetangaza kuwa uwanja wa ndege wa Bukoba utaanza kutumika tena baada ya kusitishwa kwa muda.

Operesheni za ndege zitaendelea kama ilivyokuwa hapo awali huku ndege ya kwanza ikitarajiwa kutua siku ya Jumatano.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 19 na wengine 26 kuokolewa kutoka majini katika zoezi lililoendeshwa na wavuvi wakishirikiana na maafisa polisi.

Ndege hiyo iliyokuwa ikitoka Mwanza kuelekea Bukoba ilikuwa na abiria 43 na jitihada za wavuvi na askari zilisaidia kuokoa watu 26. 

Walianza kwa kuivuta hadi karibu na ukiongo wa Ziwa Victoria ili kuwa rahisi kuitoa majini.

Mvuvi mmoja Jackson Majaliwa alituzwa kwa jitihada zake za kuwaokoa watu 24 kwenye ajali hiyo.

Alikabidhiwa shilingi Milioni moja za Tanzania (takriban Ksh 50,000) kutokana na ushupavu ambao alionyesha.

''Rais Samia Suluhu Hassan, ameagiza kijana aliyejitosa majini kuwaokoa abiria, Majaliwa Jackson, akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili apewe nafasi katika Jeshi la Uokoaji na mafunzo zaidi.''  Alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Shirika la ndege la Precision Air ndilo shirika kubwa la ndege la kibinafsi nchini Tanzania na  sehemu inamilikiwa na shirika la Kenya Airways.

Ilianzishwa mwaka 1993 na inaendesha safari za ndege za ndani na kikanda.