Mbusii na Lion wafunguka kuhusu kufanyiwa vasektomi

Watangazaji hao walikosoa utaratibu huo na kuutaja kuwa kinyume na mapenzi ya Mungu.

Muhtasari

•"Vasektomi ni utaratibu usio wa Mungu. Sikubaliani nayo. Huwezi kutumia sayansi kusimamisha ambacho Mungu alikupatia," Lion alisema.

•Mtangazaji huyo wa shoo ya jioni aliweka wazi kuwa hawezi kufanyiwa utaratibu huo kama njia ya kupanga uzazi.

Watangazaji Mbusii na Lion

Watangazaji wa kipindi cha Mbusii na Lion Teke Teke kwenye Radio Jambo, Mbusii na Lion wametoa maoni yao kuhusu Vasektomi.

Wakizungumza katika mahojiano na waandishi Samuel Maina na Caroline Mbusa, walikosoa utaratibu huo na kuutaja kuwa kinyume na mapenzi ya Mungu.

"Vasektomi ni utaratibu usio wa Mungu. Sikubaliani nayo. Huwezi kutumia sayansi kusimamisha ambacho Mungu alikupatia," Lion alisema.

Aliwahimiza wapenzi kuzingatia njia nyingine za kupanga uzazi wakisema kuwa vasektomi inaweza kusababisha majuto baadaye.

"Watu wajipange. Tumia mipira kama hutaki watoto. Huwezi kubadili vasektomi. Huko mbele ukihitaji watoto utafanyaje?" alihoji.

Lion alisema kuwa njia za kupanga uzazi kama vile matumizi ya kondomu na matumizi ya tembe za kuzuia mimba na ni chaguo bora zaidi kuliko Vasektomi.

"Vasektomi hapana!" alisema.

Mbusii alisema kuwa ni mapenzi ya Mungu kwa wanaume kuijaza dunia na sio kujaribu kuzuia nguvu zao za kiume. 

Mtangazaji huyo wa shoo ya jioni aliweka wazi kuwa hawezi kufanyiwa utaratibu huo kama njia ya kupanga uzazi.

"Hiyo haiwezi. Hata na dawa. Labda kama nimelala kabisa. Hiyo haiwezi," alisema.

Mbusii ni baba mwenye fahari wa wasichana watatu warembo na kamwe hajawahi kukwepa kufichua familia yake hadharani.

"Bibi yangu anaitwa Mama Stacy, Mama Sandra, Mama Melanny. Mimi huanika kwa sababu ni bibi yangu  na kila mtu ako na uhuru wake. Wa kuanika anaanika na wa kukosa kuanika anakosa," alisema katika mahojiano.

Aidha, watangazaji hao wameshauri vijana kujitosa kwenye ndoa wakati ambapo watajijua vizuri na watahisi wako tayari.