Mashirima awaonya mashabiki wake baada ya walaghai kutumia jina lake kuwatapeli Wakenya mitandaoni

Baadhi ya Wakenya tayari wamepoteza pesa zao walizochuma kwa bidii kupitia ulaghai huo.

Muhtasari
  • Mtangazaji huyo maarufu wa Kiswahili alishiriki picha ya skrini ya ujumbe ambao mmoja wa waathiriwa alipokea kutoka kwa washukiwa wa ulaghai

Mwanahabari mahiri Mashirima Kapombe amewaonya mashabiki wake dhidi ya walaghai mitandaoni wanaotumia jina lake kuwalaghai Wakenya.

Watu hao wasio na huruma wameunda kurasa za mitandao ya kijamii kwa kutumia picha na jina la Mashirima, ambapo wanajifanya kuendesha matangazo na kuchangisha pesa mitandaoni.

Mtangazaji huyo maarufu wa Kiswahili alishiriki picha ya skrini ya ujumbe ambao mmoja wa waathiriwa alipokea kutoka kwa washukiwa wa ulaghai.

Walimwiga Kapombe kwenye ujumbe huo na kujifanya wanaendesha promosheni mitandaoni.

Baadhi ya Wakenya tayari wamepoteza pesa zao walizochuma kwa bidii kupitia ulaghai huo.

Mwanahabari huyo alilazimika kutoa tahadhari kwa mashabiki wake baada ya kupokea malalamiko kadhaa kutoka kwa watu waliopoteza fedha zao kwa walaghai hao.

"Siendeshi matangazo yoyote, kuchangisha pesa au kadhalika. Mtu yeyote anayeomba pesa kwa jina langu ni tapeli! Kuweni makini watu wazuri'' Kapombe aliwatahadharisha wanamitandao.

Haya yanajiri baada DCI pia kuwaonya Wakenya kuwa waangalifu baada ya kuwakamata washukiwa kadhaa ambao walikuwa wakitumia majina ya Wakenya mashuhuri miongoni mwao Bibi wa Rais Rachel Ruto kuwalaghai watu mitandaoni.