Mwanablogu Cyprian Nyakundi asema makateli wanamtumia vibaya nesi Robai

Kulingana na Nyakundi, msichana huyo nesi atatumiwa na umaarufu wake utakapoisha atapotea tu akiwa maskini.

Muhtasari

• “Ilmradi anapata kulipa bili zake hakuna tatizo. Vita ni dhidi ya njaa na umaskini,” Dennis Kobare aliandika.

Nesi aliyemchezea densi mtoto mgonjwa
Nesi aliyemchezea densi mtoto mgonjwa
Image: Facebook

Mwanablogu wa muda mrefu Cyprian Nyakundi ameibuka na madai kwamba nesi aliyeonekana kwenye video akichezea mtoto mgonjwa hospitalini densi anatumiwa na walaghai wa kibiashara Nairobi kwa ajili ya kujifaidi wenyewe.

Nesi huyo kwa jina Lukresia Robai kutoka kaunti ya Trans Nzoia alitambulika baada ya video yake kusamba mpaka kumfikia gavana Natembeya aliyemuahidi kazi katika kaunti hiyo kwa kumchangamsha mtoto mgonjwa kwenye kitanda cha hospitali.

Siku kadhaa baadae, mwanadada huyo amekuwa akipokea zawadi mbalimbali kutoka kwa makampuni ya kibiashara nchini Kenya huku wengine wakimuahidi ziara ya siku kadhaa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Ndungu Nyoro, muuguzi huyo mwenye moyo mkunjufu atafurahia safari ya Zanzibar ya siku nne na usiku tano iliyofadhiliwa kikamilifu kwa hisani ya Expeditions Safaris.

Kama hilo halitoshi, juzi pia alikutana na mcheza densi wa TikTok Moya David ambaye alimpa koja la maua pamoja na hundi la pesa miongoni mwa vitu vingine vyenye dhamani ya aina yake.

Zawadi na kutambulika huku kukiendelea, wapo baadhi ya watu wanaoona kama nesi huyo anatumiwa na baadhi ya wafanyibiashara ili kujizolea faida kupitia kwa jina lake.

“Makateli wa kibiashara Nairobi wameamua kutumia huyu msichana kujizolea faida kibiashara kwa tamaa kubwa. Inakuwaje kampuni za utalii na usafiri hazijamtoa nje? Muuguzi asiye na hatia ambaye ametoka tu kutupwa kwenye magurudumu ya makampuni ya watu wa Nairobi kwa faida zao binafsi..” Mwanablogu Nyakundi alisema.

Baadhi ya watu walimuunga mkono Nyakundi huku wengine pia wakimsuta kwa kile walisema kuwa anacholenga mwanadada huyo ni kukidhi mahitaji yake kwa sababu vita ni dhidi ya njaa na umaskini na wala si kuchagua kazi.

“Anazidi kukosa umuhimu. Umaarufu wake haukuja kwa sababu ya kucheza dansi, lakini kuburudisha wagonjwa sio raia na mashirika,” Thaddius Bundi alisema.

“Ilmradi anapata kulipa bili zake hakuna tatizo. Vita ni dhidi ya njaa na umaskini,” Dennis Kobare aliandika.

“Ni faida ya pande zote kwa makampuni na yeye. Yote inategemea jinsi anavyotumia wakati huu kujitengeneza. Asipofanya hivyo, makampuni hayo yatakapomalizana naye ataanguka katika unyogovu,” Lloyd Mutua alisema.