Nameless awasuta wanaokosoa mavazi yake

Nameless alisema kuwa unyanyasaji wa mtandaoni unafaa kukomeshwa

Muhtasari

β€’ Nameless alieleza sababu ya kuwajibu wanamitandao akisema kuwa anataka liwe funzo na kuwaelimisha watu walio na fikira kama hizo mbovu.

β€’ Vilevile, Nameless aliwapongeza wanaoelewa sababu ya kuwajibu wanamitandao wanaomkemea.

Nameless
Image: Nameless Instagram

Mwanamuziki Nameless amewasuta wanamitandao wanaokosoa mavazi yake wakumtaka avae kulingana na miaka yake.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Nameless alisema kuwa watu wanafaa kukomesha unyanyasaji wa mitandaoni.

Mwimbaji huyo alieleza sababu ya kuwasuta wanamitandao kuwa anataka liwe funzo na kuwaelimisha watu walio na fikira kama hizo.

"Nahisi tunahitaji sana kusitisha unyanyasaji mtandaoni na kuhimiza huruma na hekima katika jamii kwa sababu tusipojaribu kupunguza uovu huu kwenye jamii itakuwa vigumu sana kwa watu, wewe, mimi na hata watoto wetu kustawi na kupata ukweli, faida za mitandao ya kijamii," Nameless aliandika.

Baba huyo wa watoto watatu aliongeza kuwa sababu kuu ya kutaka unyanyasaji wa mitandao kukomeshwa ni kuwa watu watakufa nyoyo na kuogopa kujieleza mitandaoni.

Alisema tabia hii isipokabiliwa ipasavyo basi watu watakuwa na ugumu kuendesha shughuli zao kwenye mitandao ya kijamii.

"Mara kwa mara baada ya muda unaweza kuniona nikijibu maoni ya ujinga kwenye ukurasa wangu na kutumia nafasi hiyo kuhimiza upendo, busara na maoni mazuri," Namless alisema.

Vilevile, Nameless aliwapongeza wanaoelewa sababu ya kuwasuta wanamitandoa wanaomkosoa kwa sababu ya vile anavyo valia.

Alisema kuwa wanamitandao walianza kumdhulumu kitambo ila alikuwa anawapuuzilia mbali kwani hakujali walichosema.

"Nimekuwa mtu maarufu kwa muda mrefu sana na kila mara nimekuwa nikikabiliana na kiwango fulani cha unyanyasaji na chuki. Kwa kweli hiyo ndiyo sababu mimi na Esir tulifanya Boomba na Maisha mnamo 2003, kwa hivyo niligundua kwamba sio kila mtu atakuonyesha upendo... Ila hayo ndiyo maisha. πŸ™πŸΏπŸ’ͺ🏾," mwanamuziki huyo alisema.