Sitaki kuwa mshindani wa kupakia picha Insta - Lynne, mpenzi wa Eric Omondi

Mwanadada huyo ameibuka wiki moja baada ya kudaiwa kupoteza ujauzito.

Muhtasari

• Nataka kuishi na kutembea katika azimio langu la ukweli. Nizidi kujisukuma ili nifikie upeo wa azimio langu - Lynne alisema.

Mpenzi wa Eric Omondi, Lynne
Mpenzi wa Eric Omondi, Lynne
Image: Instagram

Mpenziwe Eric Omondi, Lynne ameibuka baada ya sakata la kupoteza ujauzito na safari hii ameamua kuelezea ukweli wake kuhusu kinachomfanya kuendelea kubaki kwenye mitandao ya kijamii.

Lynne ameandika ujumbe mrefu wenye himizo na ujumbe kwa watu wake huku akisema kuwa uwepo wake kwenye mtandao wa Instagram si kushindana na watu katika kupakia picha na wanamtandao huo bali anataka kuishi yeye kama yeye pasi na kuangalia nini wanadada wengine wanapakia kishindani.

Mwanadada huyo alisema kwamba hatoshrutishwa wala kuingiwa na shinikizo la aina yoyote bali atakimbizana na malengo yake katika maisha pamoja pia na kuishi mpaka upeo wa kile anachokiazimia katika maisha.

“Sitaki kuwa mtu wa kushindana na wengine katika kupakia picha Instagram. Nitaka niwe mtu wa kukimbizana na malengo ya maisha yangu halisi. Nataka kuishi na kutembea katika azimio langu la ukweli. Nizidi kujisukuma ili nifikie upeo wa azimio langu, nitafanya hivi kwa neema, uadilifu na unyenyekevu,” Lynne alisema.

Vile vile alijiliwaza na kusema kwamba amejifunza katika maisha muda wote ataishi akibatasabamu hata anapopitia wakati mgumu kwa sababu hilo linampa moyo kuwa kila siku anazidi kujongea karibu na kile alichowekewa na muumba kama riziki yake.

“Nitazidi kutabasamu na kutoa shukrani hata katika ile siku mbaya kwangu, huku nikijua kuwa kila siku ninazidi kujongea karibu na riziki yangu. Kuwa na Imani na kuwaweka walio juu mbele kwa sababu bado safari ni ndefu ndefu sana,” mpenziwe Omondi aliandika kwenye Instagram yake.