(+video) Kanze Dena afanyiwa bonge la 'surprise' na waliokuwa wakifanya kazi naye ikulu

Msomaji huyo wa zamani wa habari za Kiswahili runingani alisema kuwa hajawahi fanyiwa surprise kama hilo

Muhtasari

• Jamani najiaminia kwa ma surprise…hapajatokea mtu akanifanya walivyonifanyia timu yangu ya PSCU - Mararo alisema.

Aliyekuwa msemaji wa ikulu ya rais kipindi cha uongozi wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta Kanze Dena - Mararo, alitokwa na machozi ya furaha baada ya wafanyikazi wenzake waliokuwawakifanya kazi naye ikuluni kumfanyia bonge la ‘surprise’ nyumbani kwake.

Dena ambaye kabla ya kuteuliwa kama msemaji wa ikulu na mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha kimkakati cha rais (PSCU) alikuwa msomaji wa habari za Kiswahili katika runinga ya Citizen.

Katika video aliyoichapisha kwenye mtandao wake wa Instagram, Bi Mararo, ambaye alipigwa na butwaa, alikuwa kwenye simu alipokuwa akitembea kuelekea ukumbini.

“Jamani najiaminia kwa ma surprise…hapajatokea mtu akanifanya walivyonifanyia timu yangu ya PSCU…🤣🤣 Mercy! Nashukuru jamani. Haikuwa rahisi….uwepo wenu…umoja wenu..na heshima pamoja na Mungu tulivuka. Watu wa Wizara! Pamoja tusonge mbele!! Mapenzi tele! Mungu Mbele!” Mararo aliandika huku akifurahia kwenye video ile.

Kanze alizawadiwa bango kubwa lililochapishwa na mashairi ya wimbo maarufu, Eagle When She Flies, wa Dolly Parton. Ilisherehekea nguvu, uthabiti, na ujasiri wa Kanze katika kushughulikia kazi yake.

Mwezi uliopita, Bi Mararo aliaga kazi yake katika serikali ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta huku uongozi mpya ulipokuwa ukikaribishwa.

Mtangazaji huyo wa zamani wa Citizen TV Swahili alipakia msururu wa video kuelezea safari yake katika jukumu lake kutoka maisha yake ya kibinafsi hadi ya kitaaluma.

Akiwa ametajwa kuwa msemaji wa Ikulu mwaka wa 2018, Bi. Mararo alikuwa na mazoea ya kupakia tu shughuli zake za kikazi. Hata hivyo, huku akitundika buti zake, Bi. Mararo alipakia picha za harusi yake mwaka wa 2019 iliyokuwa katika Hifadhi ya Ol Pejeta katika Kaunti ya Laikipia.