Nameless amsamehe mwanatiktoker aliyemuita jambazi

Nameless alisema kuwa dada huyo alimfuata moja kwa moja na kumtaka radhi.

Muhtasari

• Nameless alisema amekuwa akipigiwa simu ili kutoa maoni yake kuhusu alichosema mwanadada huyo kwenye TikTok; kuwa mavazi aliyovaa ni ya kijambazi.

Nameless na Imo

Mwanamuziki mkongwe Nameless amesema kuwa amemsamehe mwanadada ambaye alikejeli nguo alizovaa kwenye onyesho la kwanza la Wakanda Forever.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Nameless alisema kuwa dada huyo alitumia ujumbe akiomba msamaha maoni yake.

Alisema amekuwa akipigiwa ili kutoa maoni yake kuhusu alichosema mwanadada huyo kwenye TikTok; kuwa mavazi aliyovaa ni ya kijambazi.

"Nawashukuru kwa kunitetea mwanadada huyo alipokuwa akikejeli nguo zangu nilizovaa kuhudhuria hafla ya Wakanda Forever. Ninashukuru kwa heshima mnayonionyesha," Nameless alisema.

Baba huyo wa mabinti watatu aliongeza kuwa upendo wa mashabiki wake kwake unampa nguvu ya kuendelea kila siku.

Alieleza kuwa yeye ni mtu anayependa kuwasamehe watu iwapo wataomba msamaha au hata wakikosa, kisha kusahau ugomvi huo.

"Upendo mnaonipa unanipa nguvu ya kujikaza kama mtu maarufu na kwenye sekta yangu ya muziki. Nilimsamehe mwanadada huyo hata akabla aniombe msamaha. Kwangu, kumsamehe mtu ni kupuuzilia mbali hisia hasi ninazopata," alisema.

Alisema ana matumaini kuwa mwanadada huyo atapata funzo kutokana na tukio hilo na kukoma kuwakosoa watu.

"Natumai hataruhusu kiburi kimfanye kupuuza mambo yaliyo mema. Naelewa hamasisho la mitandaoni linaweza kuwafanya watu kuwa watu wenye dharau kwa watu wengine. Jaribu sana kuwafanyia wengine ambacho unataka kufanyiwa!" Nameless alisema.

Nameless amekuwa akipokea maoni ambayo si ya kupendeza kuhusu maisha yake kutoka kwa watumizi wa mitandao kwa muda sasa.

Mwanamuziki huyo hata hivyo amekuwa akiwakosoa watu hao na kuwaeleza huku akisema kuwa ni funzo hata kwa watu wengine wenye fikira kama hizo.

Aliwashauri watu kukomesha unyanyasaji wa mitandaoni kwani jambo hilo linaweza kumzuia mtu katika kuboresha mafanikio yake kwa uwoga wa kukosolewa na wanamitandao.