Hakuna Mwanaume Anayeweza Kumpenda Msichana Zaidi Ya Babake - Bahati

Msanii huyo alikuwa anafurahia muda mwafaka na bintiye mchanga, Malaika Bahati.

Muhtasari

• "Uhusiano Wa Wikendi Na Binti Yangu @Malaika_Bahati” Bahati aliandika.

Bahati akiwa na bintiye Malaika
Bahati akiwa na bintiye Malaika
Image: Instagram//Bahati

Mwanamuziki na mwanamuziki Bahati Kioko amepakia picha akiwa anafurahia na binti yake mchanga Malaika Bahati katika sebule yake na kusema kwamba anampenda sana mtoto wake kuliko mtu yeyote.

Kulingana na msanii huyo, mapenzi ya baba kwa binti ni ya kiwango cha juu zaidi ambacho hakiwezi kulinganishwa na kitu kingine chochote.

Bahati alisema kwamba mtu asije akakudanganya kuwa kuna mapenzi yanayozidi yale ya baba kwa bintiye, hakuna mwanaume anayeweza kumpenda binti kama baba yake, licha ya kuambiwa mara kwa mara na wapenzi wa kiume kuwa wanakupenda, lakini mapenzi yao kwa yale ya baba hayafiki.

“Hakuna Mwanaume Duniani Anayeweza Kumpenda Msichana Zaidi Ya Baba Yake 💟 Uhusiano Wa Wikendi Na Binti Yangu @Malaika_Bahati” Bahati aliandika.

Msanii huyo amekuwa akitrend kwenye mtandao wa Twitter kwa siku tatu zilizopita baada ya video ya zamani ya mkewe Diana Marua kuibuliwa akisimulia jinsi alikuwa anachumbiana na wanaume wengi.

Katika video hiyo ya zamani ambayo ilimzolea Bahati na mkewe Diana matusi ya kila rangi, Diana alisimulia jinsi ugumu wa maisha yake ya awali kabla kupatana na Bahati yalivyokuwa.

Alisema kuwa alikuwa anachumbiana na wanaume wengi, kila mmoja akichukua nafasi yake katika kuhudumia hitaji fulani ila baadae akakutana na Bahati aliyemuokoa na kumfanya mke na mama bora mpaka sasa wamebarikiwa kuwa na watoto watatu pamoja.

Licha ya masimango yote hayo, Bahati alisimama kidete na mkewe na kumtetea kwamba yeye hawezi katu kujali maisha aliyokuwa akipitia awali kwani sasa hivi wanaganga yajayo jinsi ya kuwalea watoto wao wote.

Marua na Bahati walikaribisha mtoto wao wa tatu, Malaika Bahati takribani mwezi mmoja uliopita.